WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini, RITA, umewataka waumini wa Jumuiya ya Answar Sunna Tanzania wanaoshinikiza uongozi wa juu ya jumuiya hiyo ung'oke madarakani kutulia hadi watapotoa maamuzi yao mwishoni mwa mwezi huu.
Waumini hao wa Answar Sunna wanataka uongozi wao ung'oke kwa kukiuka katiba na kushindwa kuiendesha kwa mafanikio jumuiya yao inayotajwa ni taasisi kubwa ya pili nchini baada ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania, BAKWATA.
Meneja wa Ufilisi na Udhamini wa RITA, Linna Msanga Katema, aliiambia MICHARAZO kuwa, ofisi yao inatambua kuwepo kwa mgogoro ndani ya jumuiya hiyo baina ya waumini na uongozi wao na wanaendelea kuufanyia kazi.
Linna, alisema hatua waliyofikia katika kuutatua mgogoro huo ni vema waumini kupitia kamati yao maalum wakavuta subira ili waweze kutoa maamuzi mwishoni mwa mwezi huu baada ya kukutana na kupitia vielelezo vya pande hizo mbili.
Meneja huyo, alisema tofauti na hapo awali walipokuwa wakikosa ushirikiano toka kwa viongozi wanaolalamikiwa wakiwemo Baraza la Wadhamini na Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Poli, sasa mambo ni shwari na ndio maana wanataka waumini watulie.
"Tumeshawaandikia barua kuomba watupe muda wa mwezi mmoja toka Julai 26 hadi Agosti 26, ili RITA tutoe maamuzi juu ya kinachoendelea baina ya pande hizo mbili, hivyo tunaomba waumini watulie haki itatendeka," alisema Linna.
Nao waumini hao waliofanya mkutano wao Jumapili iliyopita walitoa maamuzi ya kuvuta subiri ili kuona RITA itaamua nini, lakini wakisisitiza wanataka haki itendeke kwa manufaa ya jumuiya yao waliyodai inazidi kudumaa kutokana na uongozi uliopo.
Wakizungumza kwenye mkutano huo waumini hao waliutaka uongozi wa kamati yao inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Hamis Buguza na Katibu, Abdulhafidh Nahoda, kuendelea kufuatilia kujua RITA itaamua kitu gani na wao wameamua kuvumilia.
Mzozo wa waumini na uongozi wa jumuiya hiyo ulianza tangu mwaka juzi kutokana na madai ya ukiukwaji katiba ikiwemo kutoitishwa kwa mikutano kwa muda wa miaka 10, pamoja na kubinafsishwa mali za jumuiya hiyo bila waumini hao kushirikishwa.
Katibu wa Baraza la Wadhamini wa Jumuiya, Abdalla Lihumbi, alinukuliwa na gazeti hili wiki iliyopita akikiri uongozi wao kwenda kinyume akidai wanafanya mipango ya kupata suluhu kwa manufaa ya jumuiya yao iliyotambuliwa kitaifa mwaka 1992.
Mwisho
No comments:
Post a Comment