STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 8, 2011

Villa Squad yahaha kusaka Mil 7.2 kuianza Ligi Kuu

UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad inahaha kusaka kiasi cha Sh. Milioni 7 kwa ajili ya kuiwezesha timu yao kwenda kuianda Ligi Kuu Tanzania Bara 2011-2012 ugenini Kanda ya Ziwa, huku aliyekuwa mlezi wao, Abdalla Bulembo akisisitiza kujiweka kando katika uongozi.
Villa iliyorejea kwenye ligi hiyo baada ya kushuka daraja mwaka 2008, imepangwa kuanza mechi zake kwa kucheza na Toto Afrika siku ya uzinduzi wa ligi hiyo Agosti 20 kabla ya kuivaa Kagera Sugar ndipo irejee Dar es Salaam kucheza mechi za nyumbani.
Habari za ndani za klabu hiyo zilizothibitishwa na uongozi wake zinasema kuwa, kwa bajeti ya haraka inayotakiwa kwa timu hiyo kwenda kucheza mechi hizo mbili za awali za Ligi Kuu inahitajika kiasi cha Sh. Milioni 7.2 ambazo klabu haijui itazipata wapi kwa sasa.
Katibu wa Villa, Masoud Yasin, alisema kinachowachanganya zaidi ni kuchelewa kutolewa kwa fedha toka kwa wadhamini ambazo kwa kawaida hupitia Shirikisho la Soka Tanzania, TFF na kutoa wito kwa wadau wa soka wa Dar es Salaam hasa wakazi wa Kinondoni kuwasaidia.
"Tunaomba wadau wa soka watusaidie ili Villa tuweze kuianza ligi kwa umakini kwani tuna hali mbaya ya kiuchumi, na hasa kuzisaka fedha hizo kwa ajili ya mechi hizo mbili za kanda ya Ziwa ambapo bajeti yake ni zaidi ya Sh. milioni saba," alisema katibu huyo.
Yasin, alisema hali yao kiuchumi ni mbaya na hawajui watafanyaje katika ushiriki wao hasa baada ya mlezi wao, Abdalla Bulembo kujiweka kando akikataa hata kuzishika nafasi ambazo zipo nje ya katiba yao kama pendekezo lililotolewa na Rais wa TFF, Leodger Tenga.
Tenga alitoa pendekezo hilo wakati akitatua sakata la kuenguliwa kwa Bulembo kuwania Uenyekiti wa Villa na kuibua mtafaruku kabla ya kutulizwa kwa uchaguzi huo kufanyika kwa kuachwa wazi nafasi zilizokosa wagombea wake ikiwemo hiyo ya Mwenyekiti.
Bulembo mwenyewe alipotafutwa na gazeti hili, alikiri ni kweli hana haja ya uongozi baada ya TFF kumwekea kauzibe, ingawa alisema anasikitika na hali inayoendelea na viongozi wa soka nchini kushindwa kuonyesha dhamira ya kweli ya kuinua mchezo huo kupitia klabu ndogo.
"Sitaki hata kusikia habari za kuongoza tena, maadam TFF iliamua kunikwamisha basi mie naendelea na shughuli zangu, ila sidhani kama viongozi wa soka nchini wanania ya kuinua mchezo huu," alisema Bulembo.
Villa ni miongoni mwa timu nne zilizopanda ligi kuu toka daraja la kwanza nyingine zikiwa ni JKT Oljoro Arusha, Coastal Union ya Tanga na Moro United ya Dar es Salaam na tayari TFF imeshatangaza ratiba ya kuanza kwa ligi hiyo Agosti 20 ikishirikisha jumla ya timu 14.

Mwisho

No comments:

Post a Comment