TIMU ya soka ya Toto Afrika ya Mwanza jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimba la CCM Kirumba, jijini humo kupepetana na wageni wao Abuja FC ya Nigeria katika pambano la kirafiki la kimataifa la kujiandaa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pambano hilo la Mwanza ni kati ya mechi mbili zitakazochezwa baina ya timu hizo mbili ambazo zimeanzisha ushirikiano wa pamoja.
Kwa mujibu wa Katibu Mipango wa Toto, Hassani Kiraka, pambano jingine la timu hizo mbili litachezwa kesho kwenye dimba la Kambarage, mkoani Shinyanga.
Kiraka alisema, mbali na mechi hizo mbili kutumiwa na timu yao kukiandaa kikosi chao kwa ajili ya duru la pili litakaloanza Januari 21, pia zitatumiwa kukusanya fedha kwa za kuiwezesha Toto kushiriki vema ligi hiyo kutokana na kuwa na hali mbaya kiuchumi.
"Tunawahimiza mashabiki wa soka wa jijini Mwanza na Shinyanga ambao kwa muda mrefu hawajapata burudani ya kimataifa kujitokeza kwa wingi katika mechi hizo ikiwa sehemu yao ya kuichangia timu yetu, ili ishiriki vema katika duru lijalo," alisema Kiraka.
Alisema, uongozi wao umepania kuona Toto Afrika katika duru la pili, ikifanya vema tofauti na ilivyokuwa duru lililopita kwa nia ya kuiokoa timu yao isishuke daraja, ndio maana wameialika Abuja Fc ambayo wameanzisha ushirikiano wa pamoja baina yao.
Aliongeza, katika mechi hizo mbili benchi la ufundi la Toto lililopo chini ya John Tegete na msaidizi wake, Choki Abeid, watatafuta wachezaji wanne kutoka kikosi cha Abuja Fc, ili ikiwezekana mwakani wawasajili katika timu yao.
Toto iliyoanza duru la kwanza kwa makeke kabla ya kutetereka na kumaliza mzunguko huo ikiwa nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi, katika kikosi chake inao nyota wawili wa Kinigeria, akiwemo kinara wao wa mabao, Enyima Darlington na Chika Chimaobi Chukwu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment