STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 25, 2012

Theresia Ojade, mshindi wa tuzo ya TASWA anaizimia Simba

MWENYEWE anakiri kuwa kiu aliyokuwa nayo tangu utotoni ya kutaka kuwa nyota wa michezo nchini, ndiyo iliyomfanya ajibidiishe, kujituma na kujifunza kwa wengine waliomtangulia na katika kipindi kifupi ameanza kuona matunda yake bila ya kutarajia. Moja ya matunda yanayomfanya mchezaji huyo mkali wa timu ya mpira wa wavu ya Jeshi Stars, Theresia Ojade kujivunia ni Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike wa Wavu aliyotwaa iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini, TASWA. Theresia, alisema tuzo hiyo ambayo hakutarajia kuipata licha ya kuwa mmoja wa nyota watatu walioteuliwa kuiwania sambamba na mchezaji wenzake wa Jeshi Stars, Zuhura Hassani na Evelyne Albert wa Magereza, imempa faraja kubwa na kumtia nguvu ya kujibidiisha zaidi. Mkali huyo aliyeanza kung'ara katika michezo tangu akisoma Shule ya Msingi akicheza netiboli, wavu na kikapu, alisema hakutarajia kama ndoto zake za kung'ara katika michezo zingeanza kutimia mapema kiasi hicho. "Kwa kweli namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuanza kutimiza ndoto zangu za utotoni za kutamba katika michezo baada ya kutwaa tuzo ya TASWA," alisema. Aliongeza tuzo hiyo haimvimbishi kichwa badala yake imemuongezea morali wa kuongeza juhudi ili aje kutamba kimataifa ikiwezekana kucheza mpira wa wavu wa kulipwa kama nyota wa nchi jirani za Rwanda na Kenya. "Natamani nifike mbali katika mchezo huu, hasa kucheza wavu wa kulipwa sambamba na kuisaidia timu yangu ya Jeshi Stars itambe kimataifa," alisema. MAFANIKIO Theresia, aliyeingia kwenye wavu kwa kuvutiwa na umahiri wa dada yake, Maria Daniel na Fausta Paul aliyestaafu kwa sasa, alisema mbali na heshima ya tuzo hiyo na kitita cha Sh. Mil. Moja, pia anashukuru wavu kumsaidia mengi. Alisema, mchezo huo umemfanya hafahamike, kutembea sehemu mbalimbali na kumwezesha kumudu maisha yake na kuisaidia familia yake licha ya kupata mafunzo ya kijeshi kama askariu wa kujitolea wa JKT. "Japo mchezo huu haulipi sana nchini kutokana na kutopewa kipaumbele na kudodora kwake, ukweli umenisaidia kwa mengi kiasi najivunia kuucheza," alisema. Alidokeza kuzimika kwa mchezo huo nchini kumechangiwa na Chama chao cha TAVA kukosa ubunifu na kuandaa mashindano mara kwa mara kuuhamaisha mchezo huo na kuutaka uongozi wake kuzinduka usingizini. Theresia alisema, pia 'ubaguzi' unaofanywa na serikali na wadhamini kwa kutupia macho soka tu, ni tatizo linalodidimiza wavu na michezo mingine na kudai angekutana na Rais angemlilia atupie macho michezo yote ili kuwasaidia wenye vipaji kunufaika nayo. "Ningemuomba Rais aitupie na kuiwezesha michezo mingine ili tunayoicheza tunufaike nayo kama kwa wanasoka na kama ningekuwa Rais ningewekeza katika michezo sambamba na kuboresha huduma za kijamii hasa Afya na Elimu," alisema. FURAHA Nyota huyo anayependa kula ugali kwa samaki na kunywa juisi ya Embe, alisema hakuna kitu cha furaha kwake kama kutwaa tuzo hiyo ya TASWA na kuhuzunishwa na kifo cha mjomba wake kipenzi, Ojade aliyefariki mwaka jana. Theresia aliyejaliwa umbo la kike na sura ya kuvutia, alisema licha ya kucheza mechi nyingi, hawezi kuisahau pambano kati ya Jeshi Stars dhidi ya Prisons ya Kenya katika fainali za michuano ya ubingwa wa nchi za Afrika Mashariki. "Naikumbuka kwa namna wapinzani wetu walivyotuzidi maarifa na namna tulivyocheza na kuambulia kipigo cha aibu cha seti 3-0," alisema. Theresia ambaye hajaolewa wala kuzaa mtoto, akitamani atakapoolewa awe na watoto watatu, ni shabiki mkubwa wa Simba na Manchester United akimzimia mchezaji mwenzake wa Jeshi Stars, Yasinta Remmy. Mkali huyo anayechishwa na nguo za rangi nyeupe na nyeusi na kupenda kutumia muda wake wa mapumziko kusikiliza muziki na kufuatilia maambo ya urembo na mitindo, aliwashukuru familia yake hasa wazazi, dada yake Maria Daniel na marehemu mjomba wake Ojade. ALIPOTOKA Theresia Sylvanus Abwao Ojade, alizaliwa Januari 8, 1988 Shirati mkoani Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Mbagala Kuu jijini Dar kabla ya kujiunga na masomo ya Sekondari katika Shule ya Mwanga na kukwamia kidato cha pili kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita katika michezo aliyoicheza tangu kinda. Klabu yake ya kwanza kujiunga kuichezea ni JKT Mgulani alipokuwa mmoja wa askari wa kujitolea wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa mkataba wa miaka mitatu. Baada ya kung'ara na timu hiyo na kumalizika kwa mkataba wake alijiunga na Jeshi Stars mwaka juzi na kufanikiwa kutwaa nao mataji mbalimbali ukiwemo ubingwa wa Ligi ya Muungano wa mwaka huu. Theresia anayewazimia wasanii Lady Jaydee na Ally Kiba wanaotamba katika muziki nchini, alisema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru wachezaji wenzake na makocha waliomnoa na kumfikisha hapo alipo. Mwanadada huyo alikiri kwamba amekuwa akipata usumbufu mkubwa kwa wanaume wakware, lakini kwa kujithamini na kutambua kuwa Ukimwi upo na unaua huepuka vishawishi jambo alilotaka wachezaji wenzake na jamii kwa ujumla nao kuwa makini kwa kuepuka tamaa. Pia aliwasihi wachezaji wenzake kupendana, kushirikiana na kujibidiisha na kujituma katika mazoezi na michuano mbalimbali ili wafike mbali. Mwisho

1 comment: