|
Kapera (wa tatu kushoto waliochuchumaa) akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga |
NYOTA wa zamani wa kimataifa wa klabu za Yanga, Pan Afrika na Taifa Stars, Omar Kapera 'Mwamba' ni mgonjwa na amewaomba mashabiki wa soka kumuombea kwa Mungu.
Beki huyo aliyewahi kuwa Afisa Michezo na Utamaduni wilayani Kinondoni na Temeke kabla ya kuiongoza Pan Afrika kama Katibu Mkuu, alisema hali yake si njema baada ya kupatwa na maradhi ya kiharusi.
MICHARAZO ilimtembelea mchezaji huyo nyumbani kwake Temeke na kukumkuta katika hali isiyoridhisha, ingawa mwenyewe (Kapera) na mkewe Rukia Rashid walisema ni tofauti na alivyokuwa siku za nyuma.
Kapera alisema alianza kuugua ghafla Oktoba mwaka jana kabla ya kuzidiwa hasa alipoanza kupinda mdomo na kupoteza hisia upande wake wa kulia kutokana na kiharusi.
"Namshukuru Mungu naendelea vema kulinganisha na siku za nyuma, lakini bado naumwa kama unavyoniona na ninaomba watanzania waniombee nipate nafuu," alisema.
"Japo kuugua ni ibada bado nawaomba wenzangu msinisahau kwa maombi na dua zenu."
Kapera ambaye alikuwa mmoja wa waasisi wa Pan Afrika mwaka 1976 baada ya mgogoro ulioikumba Yanga mwaka 1975, pia aliwataka mashabiki watakaopenda kumjulia hali wawasiliane nae nyumbani kwake au kumpa pole kupitia simu yake ya mkononi ya 0713 636255.
No comments:
Post a Comment