STRIKA
USILIKOSE
Sunday, July 1, 2012
Lamata: Muongozaji anayeota kuwafunika 'madume' kimataifa
HUENDA akawa ndiye muongozaji pekee wa kike anayewapeleka puta waongozaji wengine wa kiume waliojaza nchini kwa namna anavyoifanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu.
Wengi wanamfahamu kwa jina la 'Lamata', ingawa majina yake halisi ni Leah Richard Mwendamseke, mmoja wa waandishi wa miswada na waongozaji mahiri wa filamu nchini.
Lamata, alisema aliipenda kazi hiyo tangu akiwa mtotoni na ndio maana alitumia muda mfupi kama muigizaji akiwa na kundi la Amka Sanaa lililorusha michezo yake katika kituo cha ITV kabla ya kugeukia uongozaji wa filamu.
Mwanadada huyo alisema, mara alipoosha 'nyota' kwa kushiriki igizo la 'Ndoano' alijiunga na kampuni ya RJ chini ya Vincent Kigosi 'Ray' na Blandina Chagula 'Johari' kuandaa filamu huku akijifunza uongozaji kabla ya kuianza rasmi kazi hiyo mwaka 2010.
Lamata, anayemiliki kampuni yake binafsi iitwayo 'Lamata Enterteinment, alisema kupenda kwake kuangalia filamu na kusoma vitabu vimechangia kuwa 'malkia' wa uandishi miswada na kuongoza filamu kazi aliyodai imemsaidia kwa mengi kimaisha.
Alisema mbali na Ray, pia hawezi kuwasahau Salles Mapunda na Adam Kuambiana waliomnoa sambamba na kujifunza uongozaji wa filamu kupitia njia ya mtandao kiasi cha kuwa muongozaji pekee wa kike anayeifanya kazi hiyo kama ajira rasmi.
Baadhi ya kazi alizoziandika na kuziongoza ni pamoja na Candy, All about Love, My Angel, Rude, My Princess, Tears Forever, Time After Time, Dunia Nyingine, Mke Mwema, Mr President, Chocolate, Life to Life, The Avenger, Family War na kazi zilizopo njiani kutoka za House Maid na Injinia.
Lamata anayependa kula pilau na chips kwa kuku na kunywa vinywaji laini, alisema kati ya kazi zote alizoziandika na kuziongoza zilizo bomba kwake na kujivunia ni Candy na Rude.
Mwanadada huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya zambarau na pinki, alisema kabla ya kuingia kwenye filamu aliwazimia mno Desire Washington, Mel Gibson na James Canon,
Juu ya filamu Bongo, Lamata ambaye hajaolewa wala kuwa na mtoto ingawa anatamani kuja kuzaa watoto watatu atakapoolewa, alisema imepiga hatua kubwa kulinganisha na miaka ya nyuma ila alisema wapo watu wachache wanaoikwamisha kuvuka mipaka ya kimataifa.
Alisema ni watayarishaji wabishi wasiokubali kukosolewa na kugawa majukumu ya kazi kwa wengine na wasanii wasiotambua wapo katika fani hiyo kwa ajili ya kitu gani.
Pia alisema wizi na uharamia uliokithiri katika fani hiyo na kukosekana kwa wasambazaji wengi wa kutosha ni tatizo ambalo aliiomba serikali kujaribu kuwasaidia ili wasanii wainuke kimaisha.
Lamata mwenye ndoto za kuja kuwa muongozaji wa kimataifa na kujikita kwenye biashara, alimtaja msanii Jacklyne Wolper kama msanii anayemkubali na kumuona yupo makini katika fani hiyo nchini na anayefurahia kufanya nae kazi kama ilivyo kwa Jennifer Kyaka 'Odama'.
Muongozaji huyo aliyewaasa wasanii na wadau wote wa filamu kupendana na kushikiana, alisema ukimuondoa Mungu na Yesu Kristo wengine anawashukuru kumfikisha alipo ni Ray, Wolper na Daniel Basila.
Leah Richards Mwendamseke 'Lamata' alizaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Mbeya akiwa mtoto wa mwisho wa familia ya watoto sita na alisoma Shule za Msingi Ikuti na Karobe kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari za Arage Mbeya aliyosoma hadi kidato cha pili.
Alimalizia masomo yake ya sekondari katika shule ya Wanging'ombe ya mjini Iringa na kisha kuendelea na masomo ya juu ya Sekondari Shule ya Perfect Vision kabla ya mwaka 2008 kujitosa kwenye sanaa akianzia kundi la Amka Sanaa lililotamba katika kituo cha ITV.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment