STRIKA
USILIKOSE
Sunday, July 1, 2012
Watayarishaji wengi wa filamu wabishi- Lamata
MMOJA wa waongozaji wa filamu wa kike nchini, Leah Richard Mwendamseke 'Lamata' amesema baadhi ya watayarishaji wa filamu hawataki kukosolewa katika kazi zao na kufanya filamu nyingi kukosa ubora wa kimataifa.
Pia, alisema kama watayarishaji hao hawatawadharau waongozaji na kuwathamini wasanii wanaozicheza filamu zao, huenda soko la filamu katika anga la kimataifa likapanuka na kuchuana na zile za nchi za Nigeria, Ghana na kwingineko.
Lamata, aliyasema hayo alipozungumza na MICHARAZO na kusema, licha ya kwamba waongozaji ndio wenye nafasi kubwa ya kubebeshwa lawama kazi ikiwa mbaya, ila ukweli wengi wao wanaangushwa na ubishi walionao watayarishaji wa filamu wasiopenda kuelekezwa.
Muongozaji na mwandishi huyo wa filamu, alisema wapo watayarishaji hata wakielekezwa kufanya mabadiliko katika kazi zao ili kuziboresha hukataa na kuamini wapo sahihi na kusababisha kazi nyingi kulipuliwa na kushindwa kutamba sokoni.
"Pia wamekuwa wakiwadharau waongozaji na kuwathamini zaidi wasanii bila kujua injini ya filamu kuwa nzuri ni muongozaji makini anayeweza kupangilia kazi kulingana na hadithi ilivyo na namna ya kuiboresha ili iendane na uhalisi unaosisimua," alisema.
Alisema kama watayarishaji na baadhi ya wasanii wataamua kubadilika na kufanya kazi kwa lengo la kuiinua sanaa hiyo ni wazi filamu za Tanzania zinaweza kutamba kimataifa na kuchuana na kazi za mataifa mengine ambayo wamekuwa vinara kwa miaka mingi iliyopita.
Mwanadada huyo aliyeziongoza filamu kadhaa kama 'My Princess', 'Candy', 'Mr President', 'Rude' na sasa akimalizia kazi mpya ya 'Injinia', alisema wapo baadhi ya wasanii hawajui wapo katika sanaa hiyo kwa sababu ipi kwa mambo wanayoyafanya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment