STRIKA
USILIKOSE
Sunday, July 29, 2012
Mapembe: Fundi 'mvunja mbavu' aliyejitosa kwenye muziki
TANGU utotoni, aliwavutia watoto na wanafunzi wenzake kwa kipaji cha kuchekesha, ila hakujitambua au kuota kama kipaji hicho kingemtoa kimaisha.
Ndio maana mara alipohitimu darasa la saba katika Shule ya Kiwalala, Lindi alijitosa kwenye ufundi uashi na baada umakenika katika miji tofauti.
Hata hivyo alivyotua Dar na kufanya kazi ya udereva wa daladala ndipo alipobaini alikuwa amechelewa mno, baada ya msanii Khalfan Ahmed 'Kelvin' kukitambua kipaji chake na kumshawishi kuingia kwenye sanaa.
Wengi wanamfahamu kama 'Mapembe' ila majina yake kamili ni Ismail Makomba mmoja wa wachekeshaji mahiri nchini.
Mapembe alisema wazo la Kelvin alilipuuza kwa kudhani angepoteza muda bure, lakini alipong'ang'aniwa aliamua kujiunga na kundi la msanii huyo la Simple Production na kuanza kuonyesha makeke.
Mkali huyo aliyevutiwa kisanii na Abdallah Mkumbira 'Muhogo Mchungu' alicheza kazi yake ya kwanza mwaka 2003 iitwayo 'Sheria' kisha kufuatiwa na 'Lugha Gongana', 'Talaka ya Mdundiko', 'Msela Nondo' na 'Ngoma Droo' na nyingine.
Alijitoa kwa ruksa Simple Production na kuanzisha kampuni binafsi ya Karena Production iliyozalisha filamu tano za Trafiki, Mdimu, Mbagala, Kiduku, Mpambano na sasa akijiandaa kuingiza sokoni 'Posa' akiwa pia ni muajiriwa wa kampuni ya Al Riyamy.
Mapembe ambaye pia ni mwanaharakati anajishughulisha pia na muziki akiwa ameshatoa nyimbo kadhaa na kwa sasa yupo studio kukamilisha kibao kiitwacho 'Gesi ya Kusini'.
Nyimbo zake nyingine zinazotamba hewani kwa sasa zikiwa katika miondoko ya Zouk ni Mwalimu, Nandenga, Usalama wa Raia, Muungano na Ubaya wa Mafisadi.
Mapembe anayemshukuru Kelvin na kampuni ya Al Riyamy kumfikisha alipo, anajipanga kurudi 'darasani' Chuo cha Taifa cha Sanaa Bagamoyo ,TaSUBA, ili kuongeza maarifa.
Mume huyo wa mtu na baba wa mtoto mmoja aitwae Makomba, alisema sanaa Bongo imepiga hatua kubwa, isipokuwa tatizo la wizi unaofanywa na watu wachache.
Aliiomba serikali iwasaidie wasanii kunufaika na kazi zao kwa kuweka sheria kali za kuthibiti maharamia hao, huku akiwataka wasanii wenzake kupendana na kushirikiana.
Pia aliwakumbusha wasanii wenzake wasijikite kutoa kazi zao katika nyanja za mapenzi na kusahau mambo mengine ikiwemo masuala ya kisiasa na kijamii, kama anavyofanya yeye kupitia muziki aliojitosa hivi karibuni.
Mapembe alizaliwa Januari, 1972 Kiwalala, Lindi akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Kiwalala kabla ya kujishughulisha na kazi za ufundi uashi, magari na udereva na baadae kuingiza kwenye uigizaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment