STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 27, 2012

Cheka, Nyilawila kupimwa afya uzito kesho, kuvaana PTA J'mosi

Karama Nyilawila (kushoto) na Francis Cheka wanaotarajia kupima uzito na afya kesho kabla ya kuvaana katika pambano lao lwa kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO litakalofanyika siku ya Jumamosi ukumbi wa PTA.

BINGWA wa ngumi za kulipwa anayetambuliwa na  ICB na IBF-Afrika, Francis Cheka na aliyekuwa bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyilawila wanatarajia kupima uzito na afya zao kesho tayari kwa pambano lao la Jumamosi kuwania ubingwa wa UBO-Mabara.
Mabondia hao wanatarajiwa kupambana katika pambano la uzani wa Super Middle la raundi 12 kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi.
Mratibu wa pambano hilo, Robert Ekerege wa Afrika Kabisa Entertainment, alisema Cheka na Nyilawila watapimwa uzito na afya zao sambamba na mabondia wengine watakaowasindikiza kwenye pambano lao kwenye ukumbi wa Mawela jijini Dar.
Ekerege, alisema kupimwa kwa afya na uzito wa mabondia hao ni kuashiria kuiva kwa pambano hilo la kimataifa litakalochezewa na mwamuzi toka Malawi.
"Tunatarajia kuwapima afya na uzito wao mabondia wote watakaopigana Jumamosi, karibu mabondia wote wameshatua Dar tayari kwa zoezi hilo litakaloanza kufanyika saa 5 asubuhi ili kujiweka tayari kwa mchezo huo utakaofanyika PTA," alisema.
Aliongeza kuwa, maandalizi ya ujumla wa pambano hilo la Cheka na Nyilawila ambalo ni la tatu kwao kukutana na yale ya utangulizi yamekamilika ikiwemo kubadilisha mgeni rasmi wa siku hiyo kutoka Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo , Amos Makalla hadi kuwa Kamanda wa Kanda Maalum Dar, Afande Suleiman Kova.
Ekerege alisema wamemkosa Waziri Makalla waliokuwa wamempanga awali kwa vile atakuwa safarini na hivyo kumpa jukumu la kumvika mshindi wa pambano hilo la kesho Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Kamanda Kova aliyethibitisha kushiriki.
Aliongeza kuwa katika mapambano hayo bendi maarufu ya Mashukaa Band 'Wana Kibega' ndio watakaotoa burudani ukumbini.

Mwisho

No comments:

Post a Comment