STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 20, 2012

Tegete achekelea sare za Oljoro, Azam


KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Toto Africans, John Tegete amedai kufurahishwa na vijana wake walivyopigana kiume katika mechi zao mbili za awali za ligi kuu dhidi ya JKT Oljoro na Azam na kuambulia sare tupu.
Toto iliyokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani katika mechi zote mbili, ilianza kwa sare ya bao 1-1 kwa bao la 'jioni' sawa na ilivyokuwa katika pambano lao la pili dhidi ya Azam waliotoshana nguvu ya kufungana mabao 2-2 lililochezwa jana jijini Mwanza.
Tegete alisema namna wachezaji wake walivyopigana katika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha mabao katika mechi hizo zimemfanya aamini msimu huu utakuwa wa mafanikio kwa timu yake.
Hata hivyo Tegete alisema Toto ilistahili ushindi katika mechi hiyo kama sio uzembe uliofanywa na vijana wake na kuwaruhusu Oljoro kujipatia bao la kuongoza ambalo lilikuwa likielekea kuizamisha Toto nyumbani kabla ya kusawazishwa baadae.
"Kwa kweli nimefurahishwa na namna vijana wangu walivyocheza hasa kwa kurudisha bao tulilokuwa tumefungwa, japo sijaridhishwa na bao liloruhusiwa nao na kuwafanya maafande wale kututangulia," alisema.
Juu ya mechi ya Azam alisema timu yake ilicheza vema kipindi cha kwanza kabla ya kuzidiwa maarifa kipindi cha pili, ila wachezaji walijituma na kuepuka kipigo cha mabao 2-1 kilichokuwa ikionekana dhahiri kwa mashabiki waliuofutiuka CCM Kirumba.
Tegete alisema kwa sasa akili zao zipo kwenye pambano lao la ugenini dhidi ya Coastal Union litakalochezwa Jumamosi, mjini Tanga.
Toto itavaana na Coastal ambayo imetoka mjini Mbeya ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Prisons Mbeya, huku uongozi wa timu ya Tanga wakilalamika kunyimwa bao la dhahiri lililofungwa na Atupele Green ambalo kama sio mwamuzi lingewapa ushindi wao wa pili mfululizo baada ya ule ya awali wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo JKT.

No comments:

Post a Comment