BARCELONA, Hispania
Cristiano Ronaldo aliendeleza rekodi yake safi ya kufunga magoli kwenye Uwanja wa Nou Camp baada ya kutupia mabao mawili wakati Real Madrid ikiifunga Barcelona mabao 3-1 na kutinga fainali ya Kombe la Mfalme kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2 usiku huu (Februari 26, 2013).
Straika huyo wa kimataifa wa Ureno alitupia goli la kwanza kwa penati na baadaye akaongeza la pili muda mfupi baada ya mapumziko wakati Real walipoendelea kutumia vyema mashambulizi yao ya kustukiza.
Raphael Varane akafunga la tatu katika dakika ya 68 wakati Jordi Alba akaifungia Barcelona goli la kufutia machozi katika dakika za kuelekea mwishoni mwa mechi.
Real Madrid sasa watacheza fainali na mshindi wa mechi ya kesho (Februari 27, 2013) kati ya Sevilla na Atletico Madrid. Katika mechi yao ya kwanza, Atletico walishinda 2-1.
Ronaldo sasa amefunga katika mechi zote sita zilizopita kwenye Uwanja wa Nou Camp na pia akaibuka kidedea katika vita yake binafsi dhidi ya hasimu wake Lionel Messi, ambaye 'alifunikwa' katika muda mwingi wa mechi kama walivyokuwa nyota wenzake Xavi, Iniesta, Cesc Fabregas, Pedro, Sergio Busquets na hata David Villa aliyeingia akitokea benchi katika kipindi cha pili.
Messi ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, atakuwa na nafasi nyingine hata hivyo ya kujibu mapigo ya Ronaldo wakati watakakutana tena Jumamosi katika mechi ya mzunguko wa pili wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Katika mechi ya 'Clasico' ya leo, hakukuwa na mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Barcelona huku Andres Iniesta akianzishwa katika safu ya mashambulizi badala ya David Villa na hivyo kutoa nafasi kwa Cesc Fabregas kucheza katika eneo la kiungo.
Jose Mourinho alimpanga Varane, ambaye alicheza vizuri sana katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Barca badala ya Pepe, na alishirikiana na Sergio Ramos katika safu 'ngangari' ya ulinzi ya Real Madrid na pia hakukuwa na nafasi kwa Kaka 'aliyefufuka' kivingine baada ya Angel Di Maria kuanzishwa katika nafasi ya winga wa kulia.
Barca walianza kwa kasi huku Iniesta akipiga nje kutoka umbali wa yadi 20 na baadaye Messi akapiga shuti lililopita pembeni kidogo ya lango kwa mguu wake usiotisha wa kulia wakati alipokuwa umbali wa takriban yadi sita tu kutoka langoni mwa Real Madrid. Mashambulizi hayo yalifanyika ndani ya dakika mbili za mwanzo.
No comments:
Post a Comment