Mwinyimadi Tambaza (aliyesimama) |
LICHA ya kuanza vibaya mechi za Ligi Daraja la Kwanza kwa kupokea kipigo cha bao 1-0 toka kwa Rhino Rangers, Kocha Mkuu wa timu ya Polisi Tabora, Mwinyimadi Tambaza ametamba hajakatishwa tamaa katika mikakati yake ya kuinusuru timu hiyo.
Kocha huyo alinyakuliwa na Polisi Tabora hivi karibuni kwa ajili ya duru la pili la ligi hiyo iliyoanza wiki iliyopita na kuisaidia kuiongoza kufanya vema katika mechi zao za kirafiki ikiwemo kuibana Kagera Sugar na kuzinyuka timu za Tabora Combain na Reli.
Hata hivyo katika mechi yake ya kwanza walilazwa na Rhino na juzi alitarajiwa kuiongoza tena katika pambano lao la pili dhidi ya Polisi Dodoma mechi linalotarajiwa kupigwa uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.
Tambaza alisema licha ya kwamba kipigo hicho kimetibua mipango yao ya kuvuna pointi za kutosha katika duru hilo, lakini bado wanaamini Polisi Tabora itasalia ligi hiyo kwa kushinda mechi zinazofuatia mbele yao.
"Hatujakatishwa tamaa na kipigo cha Rhino, ilitokea kama bahati mbaya kutokana na vijana wangu kujisahau lakini tumejipanga kufanya vema kwa mechi zetu zijazo, naomba mashabiki wa Polisi Tabora wasikate tamaa kwani kazi ndiyo kwanza imeanza," alisema.
Kocha huyo alisema wamerekebisha makosa yaliyowaponza mbele yua Rhino na kwamba wamepania kuanzia mechi yao ya leo kutopoteza pointi yoyote ili wamalize duru hilo katika nafasi nzuri hata kama hawatapanda Ligi Kuu msimu ujao.
No comments:
Post a Comment