STRIKA
USILIKOSE
Friday, March 1, 2013
MWANDI WAANZISHA MICHUANO YA VIJANA AFRIKA
KAMPUNI ya Tanzania Mwandi kwa kutambua kuwa Tanzania na Afrika nzima kuna vijana wengi ambao wana vipaji vya mpira wa miguu na hivyo wanachohitaji ni kuonyeshwa tu jinsi ya kuufikia ‘Ulimwengu Halisi’ wa Mpira duniani Tanzania Mwandi imeamua kuanzisha michuano ya African Youth Football Tournament ambayo itawashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 21.
Michuano hiyo itaambatana na mafunzo kwa siku tano ambapo vijana hao watapata mafunzo ya mpira wa Miguu (elimu, ujuzi na hata mbinu za uwanjani) kutoka kwa makocha wawili wa hapa nchini na watatu wa kimataifa kutoka nje ya nchi, kuanzia tarehe 10/06/2013 hadi tarehe 14/06/2013 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Aidha, mafunzo yatafanyika nyakati za asubuhi na jioni wachezaji hao watashiriki Mashindano ya kucheza wao kwa wao ili kupata vijana 11 bora miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki.
Wachezaji Bora 11 watakaopatikana watakuwa mabalozi wa Mdhamini Mkuu wa Michuano ya African Youth Football Tournament na watapata fursa ya kutangazwa zaidi kimataifa na kutafutiwa vilabu vya kucheza soka Barani Ulaya katika nchi nane (Ufaransa, Ureno, Uswis, Ubelgiji, Uholanzi, Norway, Sweden na Denmark pamoja na barani Afrika na Asia.
Ili kupanua wigo wa kuwatangaza kimataifa wachezaji wengi zaidi, Michuano hii pia itaalika skauti na mawakala wa soka wa kimataifa ili kufuatilia uwezo wa wachezaji hao asubuhi katika mazoezi na jioni kwenye michuano, kuwapata vijana bora ambao watapendelea kuwatafutia timu nje ya nchi kukipiga huko kwa makubaliano ambayo pande hizo mbili (mchezaji na wakala) zitaafikiana.
Miongoni mwa Mawakala ambao watakuwepo ni wakala wa Kimataifa wa Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro, Phillip Mwakikosa (Sweden) na wengine wengi.
Hata hivyo kutokana na gharama kubwa za uandaaji wa Michuano hii, na ndio kwanza ikiwa inaanzishwa, Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kujali mahitaji ya Kitanzania tumeweka kiingilio kwa mchezaji wa Tanzania kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300, 000) na mchezaji wa nje ya Tanzania Dola 500 za Kimarekani (USD 500).
Fedha hizo zitagharamia malazi, chakula na mahitaji mengine yote kwa mchezaji pindi atakapokuwa kambini.
Hii ni fursa adimu kwa vijana wa Kitanzania kuonyesha uwezo wao ili kutimiza ndoto za kucheza soka barani Ulaya, Asia na barani Afrika katika vilabu vikubwa huku ikikumbukwa kuwa mnamo Mwaka 2012 ni wachezaji wachache sana wa Kitanzania waliopata fursa ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kutokana na uchache wa mawakala na gharama hivyo kuletwa mawakala hao nyumbani Tanzania ni fursa pekee ya kufikia malengo.
Mpaka sasa tayari Kampuni ina majina takribani ya vijana 10 wa Nje ya nchi (Uganda, Nigeria na Ghana) ambao wameomba kushiriki hivyo tunatoa wito kwa Watanzania kutoipoteza fursa ya kuletewa njia ya kuelekea kusakata soka Barani Ulaya mlangoni mwao.
Lakini tunafahamu hali halisi ya maisha yetu kwahiyo nitoe wito kwa Wadhamini mbalimbali ambao tumewaomba kutusaidia kufanikisha Mashindano haya ambayo naamini yatalitangaza taifa letu na kulitangaza zaidi soka letu kimataifa. Pia udhamini wao utatuwezesha kupunguza hizi gharama kwa washiriki kutoka Tanzania na hivyo kuwachukua vijana wengi zaidi.
Kampuni ya Tanzania Mwandi ni Kampuni binafsi ambayo imejikita katika kuendeleza sekta za utalii, michezo na burudani ndani na nje ya nchi na hivyo kuiongezea kipato nchi moja kwa moja ama kupitia kuwawezesha wananchi kama vile kuwatengenezea fursa za ajira vijana kupitia michezo.
Fomu za ushiriki Michuano hii zinapatikana kupitia www.tanzaniamwandi.co.tz na www.blog.tanzaniamwandi.co.tz
“African Youth Football Tournament; Live your Dream.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment