STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 4, 2013

Rage: Libolo wametucheleweshea mkutano mkuu

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Rage amesema mechi yao ya marudiano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ndiyo iliyoikwamisha kamati yake ya utendaji kutangaza mapema tarehe rasmi ya mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wa klabu hiyo.
Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jijini Dar es Salaam baada ya timu yao kupoteza pambano lao la marudiano la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa goli 1-0 dhidi ya mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, timu ya Mtibwa Sugar, iliridhia kuitisha mkutano huo wenye ajenda moja tu ya kujadili mwenendo wa timu yao katika michuano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rage alisema kamati yake ya utendaji itatangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa mkutano huo muda wowote baada ya mechi hiyo kuchezwa jana. Alisema uongozi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuchezwa kwa mechi ya jana, utakuwa na wakati mzuri zaidi wa kuandaa mpango ya fedha na ukumbi ambao mkutano huo utafanyika. 
“Kwa sasa mawazo yetu yako kwenye mechi za kimataifa ndiyo maana inakuwa vigumu hata kutaja tarehe rasmi ya kufanyika kwa mkutano huo. Baada ya mechi ya leo (jana) nafikiri ndiyo tutakuwa na nafasi nzuri ya kuangalia bajeti yetu ikoje kuelekea kwenye mkutano huo,” alisema Rage.
Kamati ya utendaji ya klabu hiyo imefikia maamuzi hayo baada ya timu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’ kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika michuano mbalimbali iliyoshiriki na inayoshiriki msimu huu ikiwamo ya Kombe la Mapinduzi, ligi kuu ya Bara na Klabu Bingwa Afrika.
Wakati timu hiyo ikiendelea kusuasua katika mbio za kutetea ubingwa wake wa Bara, kumekuwa kukiibuka makundi ndani ya klabu yanayoshinikiza mwenyekiti huyo aachie ngazi kwa madai kuwa ni sehemu ya matokeo mabovu ya timu yao.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo Novemba mwaka jana huku Simba ikikumbwa na matokeo ya sare nyingi na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa, Tawi la Mpira Pesa liliibuka na kumtaka Rage kama mwenyekiti wa Simba, aitishe mkutano mkuu wa dharura ili kujadili mwenendo wa timu yao katika ligi hiyo.
Rage alipinga vikali maombi ya tawi hilo na kuamua kulifuta kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo kongwe nchini iliyoanzishwa 1936.
Simba inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu ya Bara ikiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 18 ikizidiwa kwa pointi 11 na mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame na mahasimu wao wa jadi, Yanga waliooko kileleni mwa msiamo baada ya kujikusanyia pointi 42 katika mechi 18 walizocheza.
Nafasi ya pili inakamatwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC wenye pointi 36 baada ya kushuka dimbani mara 18 pia.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment