STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 2, 2013

Aden Rage asema hang'oki Simba ng'o

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Ismail Aden Rage, amesema kuwa licha ya timu yake kufanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayoendelea nchini, hataachia ngazi hadi muda wake wa kukaa madarakani utakapomalizika mwezi Mei mwakani.
Katibu huyo wa zamani wa chama cha soka nchini (FAT sasa TFF) alisema pia anashangazwa kusikia kwamba anang'ang'ania madarakani kwa sababu anasubiria fedha (Dola 300,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 473) za mauzo ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Mganda Emmanuel Okwi zitue ili ashiriki katika mgawo wa matumizi yake.                 
Rage na viongozi wenzake waliingia madarakani mwezi Mei mwaka 2010 na kwa mujibu wa katiba, watafikia ukomo wa miaka minne ifikapo mwezi Mei mwakani.
Akizungumza na NIPASHE jana, Rage alisema kuwa kinachomfanya yeye 'apigiwe' kelele za kujiuzulu ni jinsi alivyoshiriki kudhibiti mali za klabu hiyo na kukabidhi nguvu za kisheria kwa baraza la wadhamini kama katiba yao inavyosema.
Rage alisema kuwa anafahamu kwamba suala la timu kufanya vibaya linachukuliwa kama sababu kuu lakini kilichoko nyuma ya 'pazia' ndani ya klabu hiyo ni namna baadhi ya wanachama wachache wa Simba waliokuwa wanafaidika kupitia mali za klabu kudhibitiwa na ndiyo wanaoshawishi kuwapo kwa migogoro hiyo inayoendelea chini kwa chini hivi sasa.
"Sina makosa yoyote, nilichokifanya mimi ni kurejesha heshima ya wadhamini ambao haikuwapo Simba kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, Rage siwezi kusaini mkataba wowote na hali hiyo nimeijenga ili hata nikiondoka watakaokuja waheshimu katiba ya Simba," alisema Rage.
Kuhusiana na fedha za Okwi aliyesajiliwa katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Rage alieleza kwamba siku hizi mitandao inaonyesha na kama fedha hizo zingekuwa zimeshapokelewa na kuliwa hakuna ambaye asingejua na anasikitika kuonekana kwamba yeye ndiye ana njama ya kuzitumia kwa maslahi yake binafsi.
"Tunisia kwa sasa hakuna serikali, huwezi kuhamisha fedha nje ya nchi mpaka mambo yatakapotulia, na hao wanaopia kelele wengine si wanachama na wengine hawana msaada kwa timu na hawajawahi kuichangia, ninachowaambia tuheshimu katiba," alisema kiongozi huyo ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini.
Kuhusiana na madeni mbalimbali yanayoikabili Simba hivi sasa, Rage alisema hakuna taasisi kubwa kama klabu ya Simba ambayo haidaiwi duniani na kusema pia hata wao (Simba) kuna kampuni na taasisi wanazofanyakazi nazo wanazidai lakini busara na heshima ndiyo inatumika katika kusubiri malipo yafanyike.
Alisema pia leo jioni Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo itakutana kujadili mambo mbalimbali, kubwa likiwa ni ripoti ya ufundi ya timu yao inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ya Bara.


CHANZO:NIPASHE.




No comments:

Post a Comment