Nchi ya Ghana ambayo ni moja ya nchi
zenye vipaji vingi vya wanamichezo mahiri na majina makubwa hususan mchezo wa
ngumi, itawaka moto tarehe 3, Mei wakati mabondia mahiri sita watakapogombania
mataji ya IBF katika ubingwa mbalimbali.
Bondia atakayeanza kupanda ulingoni kufukisha moto huo ni “Mtoto
wa Kijiweni” Albert Mensah ambaye amejizolea sifa kemkem za kupambana na
mabondia mahiri duniani. Mensah yuko kwenye viwango vya IBF vya dunia na
amewekwa namba 7 kwa ubora duniani katika uzito wa Welter.
Helen Joseph
Mbabe huyu atakumbana na bondia mwenye maringo na “Mtoto wa
Mjini” Ben Odamettey ambaye amekulia katika viunga vya Jamestown katika
kata ya Bukom jijini Accra, ambayo ni maarufu kwa kutoa mabingwa wengi wa dunia
kama kina Azumah Nelson, Ike Quartey, Joseph Agbeko na Poison Kotey. Wawili
hawa watapambana kugombania ubingwa wa IBF katika bara la Afrika uzito wa
Junior Middleweight.
Marriana Gulyas (kushoto)
Mpambano wa pili na unaongojewa kwa hamu kubwa ni ule wa mwanadada
na mrembo kutoka Nigeria ambaye anaishi nchini Ghaba, Helen Joseph atakapombana
na binti Mfalme kutoka Himaya ya Austrohungrian (Hungary) bi. Marianna Gulyas.
Warembo hawa wanagombania mkanda wa IBF wa Mabara wa wanawake katika uzito wa
unyoya (Featherweight) na moto mkubwa unategemewa kuwaka kutokana na umahiri wa
warembo hawa wa kurusha makonde ulingoni.
Helen atakuwa anarudisha heshina yake baada ya kupoteza pambano la
ubingwa wa dunia kwa mwanadada Dahianna Santana wa Dominican Republic mwezi wa
Desemba mwaka jana. Hii ni heshima pekee kwa kina mama kutoka bara la Afrika wa
kuonyesha umahiri wao kwa binti huyo wa Kifalme kutoka Hungary.
Albert Mensah (kulia)
Ndipo litakapokuja pambano la kukata na shoka kati ya mbabe kijana
anayeinukia katika ulimwengu wa masumbwi nchini Ghaha na Afrika kwa ujumla
bondia Issa Samir kutoka Ghana atakapopambana na mbabe kutoka kwenye
jangwa la barafu la Siberia, bondia Robison Omsarashvili kutoka katika
nchi ya Georgia ambayo ni moja ya nchi zilizokuwa kwenye Muungano wa
Kishoshalisti wa Sovieti ya Urusi (USSR).
Ni nderemo na vifijo kwa Waghana na watu wote wa Afrika wakati
mabondia hawa watakapo pambana kugombea mataji haya makubwa kabisa ya IBF na
kuliwakilisha bara la Afrika katika ramani ya dunia.
Mapambano haya yanaandaliwa na kampuni ya GoldenMike Boxing
Syndicate ya Accra, Ghana chini ya Henry Many-Spain na Michael
Tetteh na yatafanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Accra (Accra
International Conference Center) na yatasimamiwa na Rais wa IBF katika bara
la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi.
No comments:
Post a Comment