Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako |
Kikosi cha Yanga kikijifua visiwani Pemba |
Simba wakijifua mjini Unguja, Zanzibar |
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema hauna tatizo la badiliko la mwamuzi lililotangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ukidai kuwa jukumu la klabu yao ni kucheza soka na siyo kupendekeza waamuzi na kuwashangaa watani zao Simba walionukuliwa jana wakidai wanaweza kutopeleka timu uwanjani Jumamosi.
Simba kupitia Mwenyekiti wake wa Usajili, Zakaria Hanspope alinukuliwa kutokubaliana na maamuzi ya kubadilishwa kwa mwamuzi, Israel Nkongo na nafasi yake kupewa Martin Saanya wa Morogoro ili kuzihukumu Simba na Yanga katika pambano la kufungia msimu wa 2012-2013.
Hanspope ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, alisema wanahisi kuna mchezo mchafu ambao unaweza umetumika katika kubadilisha ghafla mwamuzi huyo na kwamba wangekutana mara moja ili kujadili na kuona kama wasusie mechi au la.
Hata hivyo wenzao Yanga kupitia Katibu Mkuu wake, Lawrance Mwalusako aliiambia MICHARAZO kwamba hawaoni tatizo la kubadilishwa mwamuzi kwa sababu jukumu lao wao ni kucheza soka na siyo kuamua mechi zao zichezeshwe na nani kama wanavyolilia Simba.
Mwalusako alisema huenda TFF imebaini tatizo dhidi ya mwamuzi wa awali na kufanya mabadiliko kitu alichodai huwa ni kawaida na klabu hazina mamlaka ya kuingilia kati kwa vile jukumu lao ni kucheza soka na masuala ya waamuzi ni jukumu la TFF na washirika wake katika kusimamia soka nchini.
Katibu huyo, beki wa kati wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema huenda wenzao Simba wameanza kutafuta visingizio mapema baada ya kubaini kwamba ni vigumu Jumamosi kuepuka kipigo katika pambano lao litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
"Sisi hatuoni tatizo la kubadilishwa kwa mwamuzi wa pambano letu la Jumamosi kwa sababu hayo siyo makujumu yetu, pia kwa timu iliyojiandaa vyema haiwezi kulalamikia mambo ambayo sio kazi yao, labda wenzetu walikuwa na mipango maalum na mwamuzi wa awali ndiyo maana wanalalamika," alisema.
Mwalusako aliongeza, pia inawezekana Simba wameshaanza kuingiwa mchecheto na kuamua kutafuta visingizio mapema kwa mashabiki wao pale watakapokumbana na kipigo kikali toka Jangwani.
"Wao wasihangaike kutafuta visingizio, kipigo cha Jumamosi kipo kwa vyovyote timu yetu imejiandaa vyema na ina kiu ya kulipa kisasi pamoja na kusherehesha sherehe za ubingwa wa taji la 24 katika soka ya Tanzania," alisema Mwalusako.
Juu ya kikosi chao alisema kinaendelea vyema kwenye kambi yao iliyopo Pemba visiwani Zanzibar na kwamba wanahakika ya kupata ushindi mnono kwa watani zao Jumamosi na kuwataka mashabiki na wanachama wao kujiandaa kuupokea ushindi huo kwani Simba hawachomi vyovyote ilivyo.
Yanga iliyotwaa ubingwa huo msimu huu kwa kuinyang'anya Simba ina deni kubwa la kulipa kisasi cha mabao 5-0 iliyopewa Mei mwaka jana katika mechi kama hiyo ya kufungia msimu uliopita, pia kwa miaka zaidi ya 30 imeshindwa kurudisha kipigo cha bao 6-0 walizopewa na watani zao Julai 1977.
Wakati Yanga wanajiwinda wakiwa visiwani Pemba, wenzao Simba wamejichimbia Unguja, pia Zanzibar.
No comments:
Post a Comment