STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, November 18, 2013

Huyu ndiye Jonas Mkude, mkali mwenye ndoto lukuki

Jonas Mkude (kulia) akionyesha makeke yake uwanjani

Jona Mkude kulia

Akishangilia moja ya mabao yake

Yupo Kazini (kushoto)
MWENYEWE anakiri ndoto zake za utotoni ilikuwa ni kuja kuwa Mhasibu, ila kupenda kwake soka kupita kiasi kulimfanya Jonas Mkude kusahau kila kitu na kujikita katika mchezo huo.
Kiungo-mkabaji huyo anayeichezea Simba na Taifa Stars, hata hivyo anasema anashukuru soka limemsaidia kumjengea jina kubwa na kumnufaisha kimaisha tofauti na alivyofikiria mwanzoni kiasi cha kutojuta kucheza mchezo huo.
"Siyo siri nilipenda na kutamani mno kuja kuwa Mhasibu, lakini upepo wa soka ulibadilisha mawazo yangu, japo kwa sasa sijuti kwani limeninufaisha," anasema.
Anasema ukiondoa jina kubwa alilonalo, kutwaa mataji na medali kadhaa na Simba, kuitwa kwake katika timu za taifa kuanzia U17 mpaka ya wakubwa, Mkude anadai soka limemfanya pia atembee sehemu na kufahamiana na watu na kupata marafiki wengi.
"Kwa kweli nashukuru soka limenitoa sehemu moja na kunipeleka kwingine, kubwa kunufaika kimaisha ingawa sipendi kuanika kila kitu hadharani, ila  nashukuru mno," anasema.
Mchezaji huyo aliyeanzia soka la chandimu katika timu ya Hananasif Kombaini kabla ya kunyakuliwa na Mwanza United kisha kuonwa na Simba iliyomsajili kikosi cha vijana mwaka 2010, anasema licha ya mafanikio aliyonayo katika soka, hajaridhika mpaka atakapocheza soka la kulipwa katika klabu kubwa za Ulaya.
"Kila mchezaji huota ndoto hiyo ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini mimi ningependa zaidi kucheza Ulaya katika klabu zinazotambulika," anasema.
Anasema hata hivyo ndoto hizo zitakamilika kama atapatikana wakala au mtu wa kumsaidia kufanikisha hilo, huku akiapa kupigana ili kulinda kiwango chake.
"Bila kujituma na kucheza kwa bidii ni vigumu kufika mbali, hata wenzangu nawashauri wazingatie hilo wakijikita kwenye nidhamu nzuri na kujitunza," anasema.
Akipongezwa na Amri Kiemba (28)
BAO KALI
Shabiki huyo wa Manchester United anayemzimia kiungo nyota wa Barcelona, Iniesta analitaja pambano la Ligi Kuu la msimu wa 2011-2012 kati ya Simba na Moro Utd lililochezwa Nov 5, 2011 kuwa ni pambano gumu kwake asilosahau.
Anadai anaikumbuka mechi hiyo iliyochezwa dimba la Taifa kwa vile Simba ililemewa na kuwa nyuma kwa muda mrefu kwa mabao 3-0 kabla ya kuingizwa uwanjani akitokea benchi na kusaidia kubadilisha matokeo hayao na kuwa 3-3.
"Nalikumbuka pambano hilo kwa namna nilivyoisaidia timu yangu kupata sare hiyo ya 3-3 baada ya kuingizwa kipindi cha pili nikitokea benchi, japo sikufunga lakini nilichangia upatikanaji wa mabao hayo," anasema.
Hata hivyo wakati Mkude akilitaja pambano hilo, mashabiki wa soka huenda wanamkumbuka zaidi kwa bao lake tamu linalotajwa kama bao bora la mwezi Oktoba na katika duru la kwanza la ligi kuu msimu huu dhidi ya Prisons-Mbeya.
Mkude alifunga bao hilo pekee katika mchezo huo dakika ya 62 kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la penati, baada ya beki wa Prisons Lugano Mwangama kuokoa kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Christopher Edward.
Kiungo huyo chipukizi wa Simba aliuunganisha mpira huo kwa kombora lililowasisimua mashabiki waliofurika uwanjani na kuipa Simba ushindiwa bao 1-0.
Kuthibitisha kukunwa na bao hilo, baadhi ya mashabiki walichangishana fedha na kumkabidhi kiungo huyo zawadi ya Sh 50,000, kitu ambacho hutokea nadra viwanjani.
Bao hilo ni kati ya mabao matatu yaliyofungwa na mchezaji huyo katika mechi za ligi kuu kwa timu yake msimu huu, mawili akiyafunga wakati wa pambano la ufunguzi wa ligi ya msimu huu dhidi ya Rhino Rangers lililoisha kwa sare ya 2-2.

MATAJI
Mkude anayependa kula tambi kwa samaki na kunywa soda ya Fanta, anasema kwa kipindi kifupi cha kucheza kwake soka ameshatwaa mataji manne tofauti ya Kombe la Uhai na Kinesi akiwa na Simba B, ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na taji la Super8 walipoisulubu Mtibwa Sugar mabao 4-3 fainali za mwaka jana.
Jonas Mkude akiwa na moja ya medali alizonyakua akiwa na Simba

Mkude anasema kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba ndiyo furaha yake na kuhuzunishwa siku alipozimia uwanjani katika pambano la Ligi Kuu msimu huu kati ya Simba na Coastal Union.
Kuhusu soka la Tanzania Mkude anasema kwa sasa limepanda kulinganisha na siku za nyuma hata kama Tanzania haijatamba kimataifa na kudai hiyo imechangiwa na kupewa nafasi kwa wachezaji vijana.
Anasema ili kzuidi kusonga mbele ni lazima wadau wa michezo kwa maana ya viongozi, wachezaji na wote wanaohusika katika mchezo huo kuongeza juhudi zaidi katika kuwekeza katika soka la vijana na kuwa na mipango endelevu.
"Viongozi wajali na kuthamini wachezaji ili nao wawajibika ipasavyo uwanjani huku waamuzi na mashabiki nao watimize wajibu wao na kwa uwezo wa Mungu tutafika kule tunakokuota," anasema.
Jonas Gerrard Mkude, aliyezaliwa Desemba 3, 1992 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto pekee wa familia yao anasema kwa jinsi anavyojiamini uwanjani hakuna mchezaji anayemhofia nchini.
"Sijawahi kukutana na mchezaji wa kunisumbua uwanjani, kwani najiamini naweza," anasema.
Mchezaji huyo aliyesomka Shule ya Msingi Hananasif na Kambangwa Sekondari kabla ya kulowea kwenye soka, anasema hupenda kutumia muda wake mwingi kujipumzisha na kusikiliza muziki akiwataja wasanii Ben Pol na MwanaFA ndiyo anaowazimia na kuwakubali nchini.
Mkude anasema anatakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru makocha Tom Karume, Pascal na Suleiman Matola kwa namna walivyomsaidia kufika hapo kisoka.
Pia anawasahukuru mama yake mzazi, Grace Ambrose, mjomba wake Peter Ambrose, kaka yake Athuman na wachezaji wenzake wote anaocheza nao Simba.

No comments:

Post a Comment