Stars ikijifua |
Stars itaivaa Zimbabwe badala ya Kenya (Harambee Stars) ambayo ilipangwa hapo awali.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema tayari Zimbabwe wamethibitisha kuja kucheza na Taifa Stars na wanatarajiwa kuwasili jijini leo saa tatu asubuhi.
Wambura alisema kikosi cha Zimbabwe kitakuja na jumla ya watu 30 na kuongeza kwamba maandalizi ya mchezo huo unaofanyika kwa mujibu ya Kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) yako katika hatua za mwisho.
"Sasa Stars itacheza na Zimbabwe na wameshathibitisha kukubali mechi hiyo na watatua nchini Jumatatu (leo)," alisema Wambura.
Alisema mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Uganda huku akimtaja Oden Mbaga wa Tanzania kuwa ndiye mwamuzi wa mezani na mwamuzi mstaafu wa Fifa, Mtanzania Leslie Liunda, atakuwa kamishna wa mchezo huo.
Kiingilio cha chini katika mechi hiyo ni Sh. 5,000 na cha juu ni Sh. 20,000 kwa viti vya VIP A.
Wambura alisema uongozi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wamesikitika kuikosa mechi dhidi ya Stars ambayo kiufundi timu hizo mbili zilikuwa zimeshajipanga kukutana.
Aliongeza kuwa, baada ya mechi hiyo, kikosi hicho kitaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12, mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.
Katika mashindano hayo ya kila mwaka yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati, timu ya Tanzania Bara imepangwa Kundi B pamoja na Zambia, Burundi na Somalia huku Kundi A likiwa na wenyeji Kenya, Ethiopia, Zanzibar na Sudan Kusini.
Kundi C linaundwa na mabingwa watetezi Uganda, Rwanda, Sudan na Eritrea.
Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen amelalamikia kitendo cha FKF kuizuia ghafla Harambee Stars kuja nchini kucheza mechi hiyo.
"Mwanzo tulipanga kambi ya Taifa Stars iwekwe Arusha ili wachezaji wazoe mazingira ya huko kwani kwa kiasi kikubwa yanawiana na mazingira ya Kenya ambako michuano ya Kombe la Chalenji mwaka huu itafanyika. Kenya wakakataa kucheza nasi Arusha kwa madai kwamba uwanja ni mbovu," alisema Poulsen.
"Siku tatu kabla ya mechi wanatuambia hawaji kucheza nasi wakati wametuharibia mipango. Inasikitisha sana."
No comments:
Post a Comment