Dunia Mzobora enzi za uhai wake |
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa, Mzobora aliyekuwa Kaimu Msanifu Mkuu wa gazeti la Uhuru, aliyewahi pia kuwa Naibu Mhariri wa Makala wa Mzalendo alifariki saa 12 asubuhi baada ya kuumwa ghafla usiku wa kuamkia jana akiwa nyumbani kwake.
Inaelezwa kuwa, mara baada ya kumaliza kulisimamia gazeti la Uhuru toleo la jana (Jumatano), hali yake ilibadilika na kulazimisha ndugu zake kumkimbiza hospitali ya Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kuwahishwa Muhimbili na wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake aliaga dunia.
Marehemu Mzobora, aliyezaliwa April 6, 1964 Mwandege mkoani Kigoma anatarajiwa kuzikwa mchana huu katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Binafsi niliwahi kufanya kazi na Mzobora enzi za uhai wake wakati nafanya kazi Uhuru/Mzalendo na alikuwa ni mchapakazi, mcheshi na mwanamichezo.
Licha ya ucheshi, lakini marehemu Mzobora alikuwa makini katika kazi yake na alikuwa mmoja wa 'mabosi' wangu waliokuwa wakipenda kwa kujiweka watanashati karibu muda wote kiasi kilikuwa napenda kumuita 'Papaa'.
Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Dunia Mzobora, yeye katangulia nasi tu nyuma yake na MICHARAZO inaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwa kuwataka wawe na subira.
No comments:
Post a Comment