STRIKA
USILIKOSE
Monday, November 25, 2013
Watano wamwaga wino Yanga, Yondani apongezwa
WACHEZAJI watano wa timu ya Young Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young Africans ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016).
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.
Wakati huo huo kikosi cha Young Africans leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Aidha Uongozi wa klabu ya Young Africans unampa pongezi beki wake wa kati Kelvin Patrick Yondani mchezaji bora wa mwaka 2012/2013 kwa kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya Taifa Tanzania bara (Kilimanjaro stars) inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji jijini Nairobi.
Kelvin Yondani ametambulishwa rasmi leo na kocha mkuu wa timu ya Taifa Kim Poulsen kwa waandishi wa habari katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa timu ya Taifa wanaokwenda nchini Kenya katika hoteli ya Accomondia eneo la gerezani jijini Dar es salaam.
Tunapenda kumpa pongezi kijana wetu, mchezaji wetu Yondani kwa kupewa nafasi hiyo kubwa katika timu ya Taifa, tunamtakia kila la kheri na awe kiongozi bora kwa wachezaji wenzake na kuiwakilisha vizuri nchi yetu na timu yake ya Young Africans.
Young Africans Official Website
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment