Babi alipokuwa Azam |
Babii (kulia) akiwa na kocha wake binafsi wa mazoezi ( Gym) Amir nchini Malaysia |
Abdi Kassim alipokuwa akisaini mkataba wa kuichezea UiTM Fc |
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa klabu za Mtibwa, Yanga na Azam, Abdi Kassim 'Babi' amefurahia kupata nafasi nyingine ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi baada ya kufanikiwa kusajiliwa na klabu ya Ligi Kuu ya Malaysia, UiTM Fc.
Babii anayefahamika pia kama Ballack wa Unguja, amesema kufanikiwa kurejea kwenye soka la kulipwa kwa mara nyingine ni uthibitisho kuwa soka lake bado wamo isipokuwa mizengwe ya kandanda la Tanzania ndiyo inayomfanya asipewe heshima inayostahiki.
Akizungumza na MICHARAZO toka Malaysia, Babi alisema anamshukuru Mungu kwa kutua UiTM timu inayomilikiwa na Chuo cha Teknolojia na kumuomba amuongezee umri mrefu ili atumikie kipaji chake cha soka.
Alisema kabla ya hapo tangu alipotua KMKM akitokea Azam aliokuwa ameachana nao kuna watu walikuwa wakimwekea mizengwe na kutofurahishwa na kusajiliwa kwake katika klabu hiyo, lakini alipigana na hatimaye Mungu amemfungulia neema na kupata timu hiyo ya UiTM.
Babi alisema kwa namna anavyokithamini kipaji chake na kuhakikisha anakilinda kisichuje haraka anaamini ana miaka 10 ya kuendelea kucheza kandanda.
"Naamini nina miaka kama 10 ya kuendelea kucheza kwa sababu najiamini na ninaweza soka, namshukuru sana Mungu , wazazi na wote waliopo nyuma yangu katika mafanikio na jitihada zangu za soka," alisema.
Nyota huyo kabla ya kusajiliwa Azam alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya Dong Long Tam An aliyoichezea kwa muda mfupi lakini akiifungia mabao 7.
Akiwa Azam, Babi anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye uwanja wa Taifa walipoumana na Uganda, aliifungia bao la kwanza kwenye michuano ya Kimataifa dhidi ya Al Nasir Juba waliposhiriki Kombe la Shirikisho.
No comments:
Post a Comment