Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas |
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo, walidai kuwa gari hilo dogo liligongana na lori hilo wakati likitokea Arusha likiwa limewabeba wapishi waliokuwa wanakwenda Longido kwenye sherehe za Kipaimara na harambee ya kuchangia fedha za kumalizia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Harambee hiyo ilikuwa iongozwe na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowasa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
“Nilikuwa wa kwanza kufika katika eneo la ajali, nilishiriki kutoa miili sita ya watu waliopoteza maisha yao na wengine wawili walikuwa na hali mbaya wapo hospitali, "alisema mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Sendeu Parmwat, mkazi wa Longido.
Parmwat alisema kuwa watu wote waliokufa papo hapo ni wapishi waliokuwa wakiongozwa na mtaalam wa mapishi anayejulikana kwa jina maarufu la Bonge mkazi wa jijini Arusha.
Alisema polisi walifika muda mfupi na kuanza kuchukua miili ya marehemu hao na kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.
Shuhuda mwingine, Stephano Laiser, alieleza kuwa lori lililosababisha maafa hayo lilikuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara na halikuwa na taa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo usiku wa kuamkia jana.
Kamanda Sabas alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na majeruhi pia wamelazwa hapo kwa matibabu.
“Abiria sita katika Noah yenye namba za usajili T 329AWJ, walipoteza maisha na hakuna majeruhi yeyote katika lori," alisema na kusisitiza:
" Tunaendelea na uchunguzi lakini taarifa za awali zinaonyesha kuwa Noah ilikuwa katika mwendo kasi.” Kamanda Sabas aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Hamidu Msala maarufu kama Bonge; Habibu Waziri; Faridah Ibrahim; Martha Gabriel, wakazi wa Jiji la Arusha na wengine wawili bado hawajatambuliwa.
Naye Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, alithibitisha kuwapo kwa majeruhi wawili akisema hali zao ni mbaya.
“Wako katika uangalizi wa juu, majereha ni makubwa sana mmoja yuko hoi lakini tunajitahidi kuokoa maisha yao,” alisema Muuguzi huyo na kukataa katakata kutaja jina lake akidai si msemaji wa hospitali hiyo.
NIPASHE lilishuhudia ndugu jamaa wa marehemu wakiwa katika uwanja wa eneo la kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo kufuatilia taarifa za ndugu zao hao.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment