STRIKA
USILIKOSE
Friday, December 20, 2013
Waliokufa kwa mafuriko Singida wafahamika
MIILI ya watu watano wanaohofiwa kufa maji baada gari aina ya Landrover 110 TDI walilokuwa wakisafiria kutoka Kijiji cha Doromoni kwenda makao makuu ya Wilaya Iramba yaliyopo Kiomboi kusombwa na mafuriko ya Mto Nzalala imepatikana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela miili hiyo ilikutwa maeneo ya mbugani yaliyopo kwenye mto baada ya askari wa jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi kuwatafuta watu hao baada ya kukumbwa na mkasa huo katika kijiji cha Kisimba Tarafa ya Kiomboi wilayani humo.
Kamwela alisema miili hiyo imetambulika kuwa ni ya Martha Yona (18); Mkazi wa Luono, Mkulima Youce Seif (68), na Rukia Khamisi Kipetela (32), wakazi wa Kijiji cha Tulya Wilaya Iramba.
Alisema bado wanaendelea kuwasaka watu wengine wawili ambao nao wanahofiwa kufa maji katika tukio hilo lililotokea Desemba 17, mwaka huu, saa 3:30 asubuhi baada ya gari hilo kuzimika ndani ya mto huo wakati dereva, Jafar Daud akijaribu kulivusha likiwa na abiria 15.
Vilevile, alisema wanamsaka dereva huyo kwa tuhuma za uzembe na kusababisha vifo vya watu hao.
" Dereva na utingo wake walifanikiwa kukabiliana na kasi ya mafuriko na kutoroka," alisema na kusisitiza kuwa:" Tunaendelea kumsaka na akikamatwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment