Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF), limesema kwamba kuanzia Machi 1, mwaka huu
mchezaji ambaye hatakuwa amefanyiwa vipimo vya afya hataruhusiwa kucheza
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Taarifa
ya TFF leo imesema kwamba, watatoa kwa madaktari wa klabu za Ligi Kuu
fomu maalumu za vipimo kwa wachezaji na kila mchezaji atatakiwa
kufanyiwa vipimo vyote kama ambavyo fomu imeelekeza.
“Hakuna
mchezaji atakayeruhusiwa kuendelea kucheza VPL au kuchezea timu za
Taifa kama atakuwa hajafanya vipimo hivyo. Machi 1 mwaka huu ndiyo
utakuwa mwisho wa kurejesha fomu za vipimo vya wachezaji,”imesema
taarifa hiyo ya TFF chini ya rais wake Jamal Emil Malinzi.
Aidha,
Madakatri wote wa timu za Ligi Kuu kupitia klabu zao wanatakiwa
kuwasilisha vyeti pamoja na wasifu wao (CV) TFF kufikia Februari 8 mwaka
huu.
TFF
imesema wasifu na vyeti hivyo vinatakiwa ili kuwezesha Kamati ya Tiba
ya TFF kuandaa mafunzo kwa wataalamu hao wa tiba kwa wachezaji.
No comments:
Post a Comment