Jaji Joseph Warioba |
MAELEZO
YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA KATIKA
MKUTANO WA TANZANIA CENTER FOR DEMOCRACY, KUHUSU TAFAKURI NA MARIDHIANO
KUELEKEA KATIBA MPYA: WHITESANDS HOTEL,
DAR ES SALAAM, 12 FEBRUARI, 2014
___________________________________
1.0 UTANGULIZI
Katika nchi yoyote, msingi wa
uendeshaji wa nchi unategemea Katiba ambayo ni sheria kuu. Sheria zote hutungwa
kwa kuzingatia masharti ya Katiba. Katiba huainisha misingi ya Taifa, mgawanyo
wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na
ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola. Kwa ujumla Katiba ni
makubaliano ya wananchi husika kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa
mambo mbalimbali katika nchi yao.
Kutokana na maana hiyo ya Katiba,
utungaji wake unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha wananchi
katika hatua zote za mchakato wa kupata Katiba. Kadri mchakato wa kuandika
Katiba unavyowashirikisha wananchi kwa mapana, ndivyo kukubalika, kuheshimika
na utekelezaji wa Katiba utakavyokuwa rahisi. Wananchi wanaposhiriki katika
utungaji wa Katiba, na pale matakwa yao yanapozingatiwa ndani ya Katiba,
Wananchi hao huimiliki Katiba hiyo na kuiona kuwa ni Katiba yao. Wananchi huona
hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini pia katiba hiyo huakisi utashi wao
na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti yaliyomo ndani ya Katiba.
Mchakato wa katiba kwa kadri
unavyowashirikisha wananchi, ndivyo unavyowezesha kupatikana kwa mwafaka wa
kitaifa kuhusu misingi, malengo na namna serikali na vyombo vyake
vitakavyoongoza nchi. Mwafaka huo huzaa katiba ya wananchi ambayo inaimarisha
umoja, udugu, ushirikiano na mshikamano katika Taifa kwa maendeleo na ustawi wa
jamii.
1.1 Maana na sababu za Mchakato wa Katiba
Mchakato wa Katiba hulenga kupata
Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo. Michakato mingi ya
Katiba hujumuisha Kanuni na hatua kama
ifuatavyo:
(a) kukubaliana kuhusu mambo yote yanayohitajika na kupanga
malengo;
(b) kukubaliana kuhusu vyombo vya Kusimamia na utaratibu utakaotumika;
(c) kuandaa Wananchi kwa kutoa elimu ya Katiba;
(d) kukusanya Maoni ya Wananchi wa aina zote;
(e) kushauriana na Wataalam;
(f) kujifunza kutokana na Uzoefu wa Nchi mbalimbali;
(g) kuchambua na kutathmini maoni ya Wananchi;
(h) kuandika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(i) Wananchi Kujadili Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(j) Kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Toleo la
Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(k) Bunge Maalum kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba;
(l) Wananchi kuridhia Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalum
kupitia Kura ya Maoni;
(m) kuzindua kutumika kwa Katiba Mpya;
(n) utekelezaji wa Katiba Mpya.
Utekelezaji wa Masuala na hatua
zote zilioainishwa hapo juu ndio unatafsiriwa kuwa “Mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba.”
Katika mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba unaoendelea katika nchi yetu, Kanuni na hatua hizi zimeainishwa katika
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
Msingi wa kuwa na mchakato wa
katiba ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki katika hatua zote za kupata
Katiba na hivyo kuijengea uhalali.
2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MABADILIKO YA KATIBA
Katika mchakato wa mabadiliko ya
Katiba, zipo njia kadhaa ambazo hutumika. Njia hizo ni:
(a) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba;
(b) kuunda Tume ya kuandaa
Katiba kupitia sheria zilizopo; au
(c) Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba.
2.1 Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba
Kama ilivyoelezwa hapo juu,
mojawapo ya njia za kufanya mabadiliko ya Katiba ni kwa Rais kuanzisha mchakato
huo. Katika utaratibu huu, Rais huagiza wataalamu wa kuandika katiba
kutayarisha Rasimu ya Katiba. Mara baada ya Rasimu kutayarishwa, Rais humuagiza
Waziri kuwasilisha Rasimu hiyo katika chombo cha uwakilishi. Chombo cha
uwakilishi hupewa muda maalum wa kujadili na kupitisha Rasimu hiyo bila kujali
kuwa maudhui ya Rasimu husika yanaakisi maoni au matakwa ya wananchi. Kimsingi,
katiba inayopatikana kwa utaratibu huu hutokana na utashi na matakwa ya Rais au
Serikali iliyopo madarakani. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na aliyekuwa Rais wa
Misri Bw. Morsi na pia unaendelea kutumiwa na Utawala wa kijeshi wa nchi
hiyo.
2.2 Kuunda Tume ya kuandaa
Katiba kupitia sheria zilizopo
Utaratibu mwingine wa mchakato wa
mabadiliko ya katiba hufanywa kupitia Tume inayoundwa kwa mujibu wa sheria
zilizopo ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali katika
Nchi. Chini ya utaratibu huu, Rais au Waziri mwenye dhamana ya masuala ya
katiba, kwa mamlaka anayopewa na sheria husika huunda Tume au Kamati za kushughulikia
mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Tume au Kamati inayoundwa
hupatiwa hadidu za rejea na muda maalum wa kukamilisha mchakato. Ripoti ambayo
itaandikwa kutokana na mchakato uliofanyika, hutumiwa na Serikali kuandaa
Rasimu ya Katiba au sheria ya marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, licha ya
mchakato huu kutowashirikisha wananchi kwa upana na uwazi, Serikali hailazimiki
kufanya mabadiliko yoyote ya katiba na inaweza kukalia Ripoti na kupuuza
matakwa ya wananchi.
Aidha, mchakato wa mabadiliko
unaofanywa na Tume au Kamati kupitia utaratibu huu huzingatia hadidu za rejea
zilizotolewa na Serikali, ambazo wakati mwingine haziakisi, matakwa au madai ya
wananchi. Ghana, Uganda Zimbabwe na Zambia ni miongoni mwa nchi zilizowahi
kufanya au kujaribu kufanya mabadiliko ya Katiba kwa kutumia utaratibu huu.
2.3 Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba
Utaratibu mwingine wa mchakato wa
mabadiliko ya katiba ni wa kutunga sheria mahsusi ya kushughulikia mabadiliko
ya katiba. Katika utaratibu huu, sheria inayotungwa hueleza utaratibu wa
mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Utaratibu huu ni shirikishi kwani wananchi
hushirikishwa kisheria katika hatua zote muhimu za uandikaji wa katiba yao.
Chini ya utaratibu huu, hadidu za rejea hutolewa na sheria yenyewe badala ya
Rais au Waziri. Aidha, Tume hupewa jukumu la kuratibu, kukusanya maoni ya
wananchi, kuyachambua na kutathmini maoni kabla ya kuandaa ripoti na Rasimu ya
Katiba. Mara baada ya kuandaa Rasimu ya Katiba, wananchi hupewa tena fursa ya
kutoa maoni yao kabla ya Tume au Kamati kuifanyia marekebisho na kuiwasilisha
katika Baraza au Bunge Maalum la Katiba.
Baraza au Bunge Maalum huwa na
jukumu la msingi la kuijadili na kuipitisha Rasimu ya Katiba. Katika baadhi ya
nchi kama vile Afrika Kusini, Ghana na Uganda, mchakato wa Katiba Mpya
ulikamilishwa na Bunge Maalum. Baadhi ya nchi pia hazikutumia Bunge Maalum na
badala yake, Rasimu ya Katiba ilipigiwa kura ya “Ndio” au “Hapana” baada ya
kutoka kwenye Tume au Kamati. Kwetu Tanzania, Sheria inayosimamia mchakato wa
mabadiliko ya Katiba imeainisha hatua zote tatu ambazo ni Tume kuandaa Rasimu
ya Katiba, Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba na kupitisha Katiba ambayo
itapendekezwa kwa wananchi ili kuipigia kura ya maoni.
3.0 MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA
Mwaka 2011, Taifa la Tanzania
lilianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba. Kwa mara ya kwanza katika
historia ya Tanzania, Bunge lilitunga sheria mahsusi ya kusimamia mchakato wa
mabadiliko ya katiba. Sheria hiyo inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Sura ya 83 imeweka masharti kuhusu usimamizi na uendeshaji wa mchakato wa
mabadiliko ya katiba. Sheria hii imempatia mamlaka Rais kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar.
Katika kutekeleza matakwa hayo,
Sheria ilimtaka Rais kualika Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuiya
za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya na Taasisi zisizo za Kiserikali na Makundi
ya Watu wenye Malengo Yanayofanana kupendekeza majina ya watu wanaoweza
kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume .
Sheria hiyo imeainisha utaratibu
wa utendaji kazi wa Tume na Hadidu za Rejea ambazo ni:
(a) kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi;
(b) kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya
kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala
wa sheria na utawala bora;
(c) kutoa mapendekezo kwa kila Hadidu ya Rejea; na
(d) kuandaa na kuwasilisha Ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Sheria hiyo pia, inaainisha
Misingi ya Kitaifa na Maadili ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Tume katika
mchakato wa kupatikana Katiba Mpya. Misingi hiyo ni:
(a) kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) uwepo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
(e) umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(f) uchaguzi wa kidemokrasia na wa mara kwa mara katika vipindi
maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
(g) ukuzaji na uhifadhi wa Haki za Binadamu;
(h) utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria; na
(i) uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote
na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
Kwa ujumla, Sheria inaainisha
kazi na majukumu ya Tume kuwa ni:
(a) kuandaa na kuendesha programu za elimu kwa umma juu ya
madhumuni na majukumu ya Tume;
(b) kuitisha na kusimamia mikutano au Mabaraza ya Katiba katika
sehemu na nyakati mbalimbali kama itakavyoamua;
(c) kutathmini na kuchambua maoni ya wananchi yanayokubaliana na
yale yasiyokubaliana; na
(d) kutayarisha na kuwasilisha Ripoti kwa kuzingatia Hadidu za
Rejea.
Katika kutekeleza kazi na
majukumu yake, Tume imepewa mamlaka ya:
(a) kumtaka mtu yeyote, atakayehiari, kwenda mbele yake na
kufanya naye majadiliano kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka;
(b) kupitia na kufanya uchambuzi wa michango, mawazo, maoni,
taarifa na mapendekezo yaliyotolewa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma,
kupitia nyaraka mbalimbali zilizoainishwa katika Sheria hiyo, na nyingine zozote
ambazo Tume itaona zinafaa;
(c) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za
Mitaa, Afisa Mtendaji wa Kata au Afisa Mtendaji wa Kijiji kuitisha mkutano wa
Wakazi wa Mji, Kata, Mtaa au Kijiji kwa Tanzania Bara;
(d) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Katibu wa
Halmashauri ya Mji au Wilaya, au Sheha kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji au
Shehia, kwa upande wa Zanzibar;
(e) kuunda Kamati kwa ajili ya kazi za jumla au maalum;
(f) kumtumia au kumshirikisha mtaalamu mwelekezi au mtu yeyote
kadri itakavyokuwa lazima; na
(g) isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, kutumia
utaratibu unaofanana wa ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wananchi,
uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba na uandaaji wa Ripoti.
Sheria pia imeainisha kuwepo kwa
Bunge Maalum la Katiba na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, utaratibu
wa kuwapata Viongozi na Sekretarieti ya Bunge Maalum la Katiba umeainishwa
katika Sheria hii. Sheria pia imeainisha utaratibu wa Bunge Maalum kuandaa na
kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na Utaratibu wa Majadiliano ya
kupitisha Rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kwa Wananchi ili kuipigia kura ya
maoni. Katiba itapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka
Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka Zanzibar. Utaratibu wa kura
ya maoni na Uzinduzi wa Katiba mpya pia umeainishwa.
Kwa kifupi, Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba, Sura ya 83, ni Katiba au Msahafu wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba
unaoendelea hivi sasa. Sheria imeunda vyombo vyote muhimu na kila chombo
kimepewa hadidu za rejea. Kila chombo kimewekewa utaratibu wa kazi na madaraka
yake. Katika utaratibu huu kila chombo kina madaraka yake yaliyowekewa mipaka.
Haiyamkini kwa Tume kukusanya maoni, kuandika Rasimu ya Katiba, kuiwasilisha
katika Bunge Maalum la Katiba kisha nayo ishiriki kuijadili Rasimu ya Katiba.
Au, Bunge Maalum la Katiba, lenye madaraka ya kujadili na kupitisha Rasimu ya
Katiba wakati huo huo kuandika Rasimu ya Katiba mbadala au kubadili mfumo wa
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Hivyo hivyo, kwa Tume ya Uchaguzi na
Wananchi. Kila aliyetajwa, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano na
Rais wa Zanzibar, ana jukumu maalum lililoainishwa na Sheria.
4.0 WAPI TULIPO HIVI SASA
Kufuatia Tume kukabidhi Ripoti na
viambatanisho vyake kwa Marais, kama Sheria inavyoelekeza Rais
amekwishachapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Gazeti la
Serikali na vyombo vingine vya habari, amekwishateua Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba na kuliitisha Bunge Maalum la Katiba ili kukutana kuanzia tarehe 18
Februari, 2014, Dodoma. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba katika
Bunge Maalum. Bunge hilo litakuwa na wajibu wa kujadili na kupitisha Rasimu ya
Katiba kabla ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
5.0 BUNGE MAALUM NA MAJUKUMU YAKE
Bunge Maalum la Katiba ni chombo
cha uwakilishi kama lilivyo Bunge la kawaida isipokuwa Bunge Maalum la Katiba
huundwa kwa ajili tu ya kutunga Katiba na kufanya shughuli zingine zinazoambata
na utungaji wa Katiba. Bunge Maalum la Katiba hupewa jukumu hili la kutunga
katiba badala ya Bunge la kawaida kwa sababu Bunge Maalum la Katiba
linawakilisha wananchi ambao ndio msingi wa mamlaka ya nchi na vyombo vyake
vyote ikiwemo Bunge la kawaida ambalo pia ni zao la Katiba.
Majukumu ya Bunge la Maalum la
Katiba yanaweza kutofautina kulingana na namna utaratibu mzima wa mchakato wa
mabadiliko ya katiba ulivyopangwa. Katika baadhi ya nchi, Bunge Maalum la
Katiba hupewa mamlaka ya kusimamia mchakato wote wa mabadiliko ya katiba,
wakati katika nchi nyingine Bunge hili hushirikiana na vyombo vingine katika
kufanya na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.
5.1 Madaraka ya Bunge Maalum
Madaraka ya Bunge Maalum yamekuwa
yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika kusini, Namibia na Cambodia Bunge
Maalum lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika
mazingira haya, Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi
katika Rasimu ya Katiba. Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kuachana na
Rasimu ya Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
Madaraka ya Bunge Maalum yanakuwa
na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko ya Katiba au
Chombo cha aina hiyo. Bunge Maalum linaweza
kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba
lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa
wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya
madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalam wa masuala ya Katiba, wanaeleza
kuwa madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya
Katiba.
Kwa mujibu wa kifungu cha 25(1)
cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge Maalum limepewa madaraka
ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria ya Masharti ya
Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge Maalum
litapitisha Kanuni za Bunge Maalum ambazo zitaongoza utekelezaji wa mamlaka ya
Bunge Maalum.
5.2 Kanuni za Bunge Maalum
Kanuni za Bunge Maalum la Katiba
sharti zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini
ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya
Katiba.
Katika kutekeleza madaraka ya
kujadili na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi
kwamba masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto
za Wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi
ya wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya Watu Wenye Malengo
Yanayofanana.
Bunge Maalum litafanya kazi ya
kuboresha masharti ya Kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka
masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya
kikatiba yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
6.0 MUUNDO WA MUUNGANO WA
SERIKALI TATU
Muundo wa Muungano umewekwa
katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Ili kupata maana kamili ya muundo wa
Muungano unaopendekezwa, Tume ni vema kusoma Sura ya Kwanza, Sura ya Nane na
Sura ya Kumi na tano.
Taswira ya Muungano wa Serikali
Tatu unaopendekezwa katika Rasimu ya Katiba imejengwa katika Ibara ya 1 inayoieleza
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili
– Sovereign Federal Republic. Kwa hali hiyo Muungano wa Serikali Tatu haubadili
hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya ya kimataifa kuwa ni nchi moja.
Kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika haina maana ya kuunda nchi
mpya. Kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya Mambo ya Muungano na Mambo
yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.
Tanganyika na Zanzibar hazina hadhi ya Jamhuri, na kwa hiyo si
“Sovereign States” kama ilivyo Jamhuri ya Muungano.
6.1 Misingi ya Muundo wa Muungano wa
Serikali Tatu
Muungano wa Serikali Tatu
unaopendekezwa umezingatia mamlaka tatu zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano
hivi sasa:
(a) Mamlaka ya Mambo ya
Muungano –Jurisdiction on Union Matters yanayosimamiwa na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4(2), (3) na 34(1) na (3) za Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
(b) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar
yanayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na (3), 64(2) na (5) na
Ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na
(c) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika ambayo kwa
sasa yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa - Ibara
ya 4, 34(2) na (3) na 64 (4).
Kila mamlaka sasa itakuwa na
Serikali yake ambayo itasimamiwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
6.2 Mgawanyo wa majukumu na
madaraka katika Serikali tatu
Ibara ya 60 na Nyongeza ya Kwanza
inaorodhesha mambo saba ya Muungano ambayo yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano.
Haya ndiyo masuala makuu na ya msingi ya kidola (Sovereign Functions) ambayo
ndiyo yalivyo katika masuala 11 ya Muungano yaliyomo katika Hati ya Muungano ya
Mwaka 1964.
Katika mambo haya saba, Jamhuri
ya Muungano inayo mamlaka kamili tena yasiyogawanyika. Mambo hayo 7 hayawezi
kufanywa na Serikali za Nchi Washirika wa Muungano kwa sababu hazina sifa ya
“Sovereign States”. Kwa mfano suala la ulinzi na usalama lipo moja kwa moja
katika Jamhuri ya Muungano. Pamoja na orodha ya mambo ya Muungano
yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza, zipo taasisi ambazo zimetajwa
katika Rasimu ya Katiba kuwa za Muungano lakini hazijaorodheshwa. Taasisi hizo
na mambo hayo yamejumuishwa katika Mambo ya Muungano Yaliyokusudiwa katika aya
ya 1 ya Mambo ya Muungano, yaani – Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
6.3
Hadhi ya Marais wanaotajwa katika Rasimu ya Katiba
Katika Rasimu ya Katiba yumo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar.
Ingawa wote wanaitwa Rais, lakini hawafanani kwa hadhi na majukumu. Rais mwenye
mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano ni Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo,
kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba, Rais wa
Jamhuri ya Muungano ndiye peke yake Mkuu
wa Nchi mwenye mamlaka kamili (Head of State), Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa
Serikali ya Muungano. Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar hawana sifa hizo
ingawa wao ni wakuu wa mambo yote yasiyo ya Muungano katika maeneo yao ya
utawala. Kwa kuhakikisha hilo, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar
hawakupewa hadhi ya Makamu wa Rais kwa makusudi. Kwa msingi huo hawawezi
kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano akisafiri au akiwa hawezi
kutekeleza kazi kwa muda. Hilo likitokea wanaweza kukaimu ni Makamu wa Rais,
Waziri Mwandamizi, n.k.
6.4 Misingi ya utendaji ya Muungano wa Serikali Tatu
Muundo wa Serikali Tatu umejengwa
katika Misingi ya Utendaji (Principles) ifuatayo:
(a) Muungano wa Hiari (Voluntary Union);
(b) ushirikiano ( Co-operation);
(c) uratibu (Co-ordination);
(d) Mshikamano (Solidarity); na
(e) subsidiarity.
6.4.1 Muungano wa Hiari (Voluntary Union)
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar. Msingi wa Muungano huu ni Makubaliano ya Muungano (Articles of Union)
ya mwaka 1964 yaliyofikiwa baina ya mataifa haya mawili. Chini ya makubaliano
hayo, mataifa hayo yalikubaliana kwa hiari kuachia baadhi ya mamlaka na
kuyapeleka mamlaka hayo katika Serikali ya Muungano. Uhiari huu wa kukubali
kuungana kwa mataifa haya mawili ni moja ya misingi ya utekelezaji wa muundo wa
Muungano unaopendekezwa wa Serikali Tatu. Ibara ya 1(3) ya Rasimu ya Katiba
inapendekeza pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano iwe ni msingi mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.4.2 Ushirikiano (Co-operation)
Msingi mwingine wa utendaji
katika muundo wa Serikali Tatu ni Ushirikiano. Chini ya msingi huu, Serikali ya
Muungano na Serikali za Nchi Washirika zitakuwa na ushirikiano baina yao katika
shughuli zote za utendaji na uendeshaji wa nchi ili mradi ushirikiano huo
haukiuki Katiba. Ibara ya 65(1) inapendekeza kuwa Nchi Mshirika iweze kuomba
ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha
uhusiano wake wa kikanda au kimataifa. Aidha, Ibara ya 66 inapendekeza masharti
kuhusu ushirikiano kati ya Nchi Washirika zenyewe na baina ya Nchi hizo na
Serikali ya Muungano kwa lengo la kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na kukuza
maendeleo ya wananchi.
6.4.3 Uratibu (Coordination)
Katika mfumo wa Serikali Tatu,
uratibu wa uhusiano baina ya Serikali hizo ni moja ya misingi muhimu. Ibara ya
67 inapendekeza kuwepo kwa Waziri Mkaazi atakayeteuliwa na kila Nchi Mshirika atakayefanya
kazi akiwa Makao Makuu ya Serikali ya Muungano. Moja ya majukumu ya msingi ya
Waziri Mkaazi ni kuratibu uhusiano baina ya Serikali yake na Serikali nyingine
ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya Muungano. Aidha, Ibara
ya 109 inapendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali
chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais. Kuwepo kwa uratibu kutaimarisha uhusiano
wa kiutendaji baina ya Serikali zinazopendekezwa na hivyo kuimarisha Muungano.
6.4.4 Mshikamano (Solidarity)
Mshikamano (Solidarity) ni moja
ya misingi muhimu ya utendaji katika mfumo wa Shirikisho. Msingi huu
umezingatiwa katika Rasimu inayopendekezwa ili kuhakikisha kuwa Serikali zote
tatu zinashikamana na kusaidiana katika kila hali inayoweza kujitokeza. Mathalani,
Ibara ya 62(3) inapendekeza kuipa Serikali ya Muungano, kwa makubalino na
masharti maalum na Serikali ya Nchi Mshirika, madaraka ya kutekeleza jambo
lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Nchi Mshirika. Aidha, Ibara ya 65
na 66 zinapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya Serikali za Nchi washirika
na kati ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Msingi huu ni muhimu katika
kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika kwa usawa
na mshikamano baina ya Nchi Washirika.
6.4.5 Subsidiarity
Msingi wa subsidiarity unakusudia
kuweka utaratibu wa mamlaka za chini kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya uwezo
wake ikiwa mamlaka hizo zina uwezo wa kutekeleza majukumu hayo kwa ukamilifu.
Msingi huu wa subsidiarity unaruhusu mamlaka ya juu kutekeleza jambo ambalo kwa
kawaida hutekelezwa na mamlaka ya chini iwapo mamlaka ya juu ina uwezo wa
kutekeleza jambo husika kwa ufanisi au vinginevyo. Ibara ya 65 na 66 zimeweka
msingi kwamba, ingawa Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kushughulikia
Mambo ya Muungano, Serikali hiyo, kwa ridhaa ya Serikali ya Nchi Mshirika,
itakuwa na mamlaka ya kushughulikia masuala yasiyo ya Muungano katika Nchi
Mshirika. Msingi huu utasaidia kuimarisha utendaji katika muundo wa Serikali
Tatu unaopendekezwa.
6.5 Vyombo vya kikatiba vinapendekezwa kusimamia Misingi ya
Utendaji
Katika kuhakikisha kuwa Muungano
unaimarika, Vyombo vipya vya kikatiba vimependekezwa kusimamia Misingi ya
Utendaji. Vyombo hivyo ni:
(a) Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali;
(b) Mawaziri Wakaazi;
(c) Mahakama ya Juu;
(d) Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
6.5.1 Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali
Tume ya Uratibu na Uhusiano wa
Serikali inaanzishwa na Ibara ya 109 na Makamu wa Rais atakuwa ndiye
Mwenyekiti wa Tume hii, na wajumbe wake
watakuwa ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi na Waziri
mwenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tume hii,
pamoja na mambo mengine, itakuwa na dhima ya kusimamia na kuratibu uhusiano
baina ya Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo na Serikali ya
Muungano. Tume hii ambayo inapendekezwa kuwa na Sekretarieti ya wataalam wa
fani mbalimbali, itakuwa pia na jukumu la kuwezesha uratibu na ushirikiano
katika kutekeleza masharti yanayopendekezwa na Rasimu ya Katiba, sera, sheria,
mipango na mikakati baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za
Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo.
6.5.2 Mawaziri Wakaazi
Waziri Mkaazi ni nafasi ya
madaraka inayopendekezwa na Ibara ya 67. Waziri Mkaazi atakuwa na wajibu wa
kuratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali yake na Serikali nyingine ya
Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
6.5.3 Mahakama ya Juu
Mahakama ya Juu ni chombo kingine
kinachopendekezwa kuanzishwa katika Rasimu inayopendekezwa. Mahakama ya Juu,
pamoja na mambo mengine, inapendekezwa kuwa na mamlaka ya kushughulikia
kusikiliza na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika au baina ya Nchi Mshirika
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mamlaka haya ya Mahakama ya Juu yanakusudia
kusimamia misingi ya utendaji katika muundo wa Muunganounaopendekezwa
6.5.4 Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Baraza la Ulinzi na Usalama la
Taifa linapendekezwa kuanzishwa na Ibara ya 237 ya Rasimu inayopendekezwa. Baadhi
ya Wajumbe wa Baraza hilo litaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ni
Makamu wa Rais, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Baraza hili litakuwa
ndicho chombo pekee kitakachowakutanisha Wakuu wa Serikali Tatu
zinazopendekezwa na kitakuwa chombo cha juu cha kusimamia misingi ya utendaji
katika muundo wa Serikali unaopendekezwa.
No comments:
Post a Comment