STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 18, 2014

Saleh Tendega: Kipa wa Mgambo JKT aliyewanyamazisha Simba Mkwakwani




LICHA ya sifa nyingi kuelekezwa kwa mshambuliaji Fully Maganga aliyefunga bao pekee lililoizima Simba katika Uwanja wa Mkwakwani, lakini yupo mtu mmoja aliyefanya kazi kubwa kuinyong'onesha Simba jijini Tanga.
Saleh Tendega, katika nafasi yake ya ukipa ndiye aliyeng'ara katika pambano hilo na aliyekuwa 'mwiba' mkali kwa washambuliaji nyota wa Simba kuanzia kinara wa mabao, Amisi Tambwe, Haruna Chanongo, Ali Badru hadi kwa Ramadhani Singano 'Messi'.
Kipa huyo wa Mgambo JKT, katika mechi hiyo alikuwa na kazi moja tu kuhakikisha lango lake hazitikiswi nyavu kama walivyofumaniwa katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam mwaka jana walipocharazwa mabao 6-0.
Ingawa katika mechi hiyo ya awali yeye hakukaa langoni, lakini kipigo ilichopewa timu yake bado alikuwa akikikumbuka na hivyo kucheza 'jihad' na kuwakatisha tamaa vijana wa Zdravko Logarusic na hatimaye kulipa kisasi.
Tendega, aliyewahi kuichezea Simba Kids wakati ikinolewa na kocha Mwinyimadi Tambaza, aliyemtoa nafasi ya ushambuliaji hadi katika ukipa, anasema anajisikia faraja kuisaidia timu yake kuizima Simba Mkwakwani.
"Nimejisikia furaha kwa sababu tumeweza kuchukua pointi tatu tulizokuwa tukizipigania ili kutusaidia katika safari yetu ya kuepuka kushuka daraja," anasema.
Nyota huyo anasema pamoja na kuwatungua Simba, lakini anakiri timu hiyo ni nzuri na yenye wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa kisoka na kuitabiria wanaweza kumaliza katika nafasi nzuri kama watakomaa kwa mechi zao zilizosalia.
"Simba ni timu nzuri na yenye watu wa mpira, sema hawakuwa na bahati kwetu na wana nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa, wasikate tamaa kwa kipigo tulichowapa," anasema Tendega anayeishabikia Manchester United.
Tendega akijiandaa kwenda mazoezini
FURAHA
Tendega aliyewahi kuzichezea timu kadhaa ikiwamo Ashanti United, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama kufanikiwa kulamba ajira jeshini mbali na mambo mengine aliyovuna katika soka.
"Kupata ajira jeshini kwa sababu ya soka ni jambo la furaha kwangu, na kwa huzuni nalizwa sana na vifo vya wazazi wangu, kila uchao nawaombea kwa Allah awarehemu," anasema.
Kipa huyo anayependa kula ugali kwa samaki, nyama za kuchoma au za kukaanga anasema soka pia limemwezesha kupata elimu yake ya sekondari kabla ya kumpa ajira anayodai inampa faraja na furaha kubwa maishani.
Anasema pamoja na mafanikio makubwa aliyopata katika soka bado hajaridhika na badala yake atazidi kuongeza bidii ili afike mbali zaidi.
Kuhusu soka la Tanzania, Tendega anasema lipo vema isipokuwa anataka juhudi zaidi ziongezwe kuanzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hadi kwa serikali kujitolea kuwekeza katika soka la vijana alilodai ndiyo mtaji mkuu.
"Lazima kuwapo kwa juhudi na kusaidia kujengwa kwa vituo vya soka kwa vijana na kila klabu kuwa na 'akademi' ya vijana, kama wafanyavyo Ujerumani na hata Uganda ambao leo wametuacha mbali kisoka," anasema Tendega.
Anasema pia kungejengwa shule maalum za kukuzia vipaji vya michezo ikiwamo soka ili kuzalisha nyota wa baadaye watakaolisaidia taifa kutokana na ukweli kwamba imebainika Tanzania ina vipaji, lakini hawana misingi mizuri.
Pia anasema ni vema viongozi wa kandanda nchini wakaondoa ubinafsi na kujali maendeleo ya mchezo huo ili Tanzania ifike mbali katika michuano ya kimataifa badala ya kuwa wasindikizaji kwa miaka mingi na kufarijiana tu.
Kipa huyo anayedai hakuna mshambuliaji yeyote anayemnyima raha dimbani, anaishukuru familia yake inavyomsapoti mpaka sasa, kocha aliyemjengea msingi wake kisoka, Mwinyimadi Tambaza, Joseph Kanakamfumu aliyemnoa akiwa Sekondari ya Makongo na wote waliomfundisha au kumsaidia kufika alipo sasa.
Tendega akiwa katika pozi
ALIPOTOKA
Saleh Ibrahim Tendega, alizaliwa Agosti 24, 1989 jijini Dar es Salaam. Shule ya Mtendeni alipoanza kuonyesha umahiri wake dimbani akiwa darasa la tatu akicheza kama mshambuliaji na timu ya chandimu ikiwa ni Kajima Rangers.
Baadaye alienda kujiunga na Simba Kids chini ya kocha Tambaza aliyemtoa mbele na kumrudisha golini, baadaye alihamia Yetu Afrika ya Vingunguti na kushiriki nao ligi mbalimbali wilayani Ilala kabla Villa Squad kumnyakua.
Villa ilimnyakua kabla ya kwenda Makongo Sekondari alipozidi kuimarika katika soka na baadaye kunyakuliwa na Ashanti United kisha kutua Ruvu Shooting, JKT Ruvu na baadaye Mgambo JKT alionao mpaka sasa.
Juu ya mechi ngumu anayoikumbuka, Tendega anautaja mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu 2007 kati ya timu aliyokuwa akiidakia ya Ashanti United dhidi ya Yanga, ambapo Ashanti waliiduwaza Yanga kwa kuwalaza bao 1-0.
"Naikumbuka siyo kwa ushindi tuliopata, ila kwa vile ilikuwa mechi yangu ya kwanza kubwa, pia kipindi hicho nilikuwa mdogo mno, lakini nilionyesha uwezo wa hali ya juu na kuizuia Yanga iliyokuwa ikitisha enzi hizo," anasema.
Anasema juhudi zake zilizowashangaza mpaka viongozi wake katika mchezo huo, alipochaguliwa kuwa nyota wa mchezo (man of the match) kitu kilichompa faraja na kumuongezea morali ya kujituma zaidi.
Tendega ambaye hajaoa wala kuwa na mtoto, anawaasa wachezaji wenzake kujituma, kuzingatia nidhamu na kumtegemea Mungu kwa kila jambo sambamba na kuwa na kiu ya maendeleo ili wafike mbali na mahali walipo sasa.
Kipa huyo anayependa kutumia muda wake wa ziada kuangalia muvi na kulala kumpumzisha mwili wake, anasema pamoja na Mgambo kuwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini wachezaji wamepanga kuipigania ili kucheza Ligi Kuu mssimu ujao.

No comments:

Post a Comment