MADRID, Hispania
MWANASOKA bora wa dunia, Cristiano Ronaldo amedhihirisha kuwa ni mtu
mwenye huruma baada ya kujitolea kulipa gharama za upasuaji wa mtoto
mwenye umri wa miaka 10.
Mtoto huyo, Erik Ortiz Cruz, anasumbuliwa na matatizo mbalimbali ya
kiafya na upasuaji ndio pekee utakaoweza kunusuru maisha yake.
Familia ya mtoto huyo imeshindwa kumudu gharama za matibabu ya mtoto
huyo hospitali, ambapo gharama za kila kipimo ni pauni 5,020 za
Uingereza na upasuaji ni pauni 50,240.
Kutokana na hali hiyo, Ronaldo ameguswa na jitihada zinazofanywa na
familia hiyo kwa ajili ya kukusanya fedha za kulipia matibabu ya mtoto
huyo na kuamua kubeba mzigo huo.
Awali, Ronaldo aliombwa kuchangia viatu na fulana ili vipigwe mnada kwa
ajili ya kuchangia fedha za matibabu hayo, lakini aliamua kwenda mbali
zaidi kwa kulipa gharama hizo.
Mapema mwaka huu, Ronaldo alisherehekea tuzo ya kuwa mwanasoka bora
duniani na watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kansa, akitekeleza ahadi
aliyoitoa mwaka jana alipohojiwa na kituo cha redio cha Hispania.
Ronaldo alikutana na watoto hao wakati wa kipindi cha redio hiyo cha
Partido de la 12 Novemba mwaka jana na kusema, iwapo atashinda tuzo
hiyo, atasherehekea nao.
No comments:
Post a Comment