ROHO zikiwadunda baadhi ya mashabiki wa kandanda nchini kuhuisiana na pambano la marudiano baina ya Yanga na Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha msaidizi wa mabingwa hao watetezi wa Tanzania, Charles Mkwasa amesisitiza timu yao haitapaki basi badala yake itashambulia mwanzo-mwisho.
Yanga inavaana na Alhy wiki moja baada ya kuwadonyoa bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo katika mechi ya leo Jangwani wanahitaji sare yoyote ili kufuzu hatua ya 16 Bora.
Mechi hiyo inachezwa kwenye uwanja wa Mexx, mjini Alexandria badala ya Cairo kama ilivyokuwa ikifahamika awali, kitu kinachoelezwa kama hila za wapinzani wao kutaka kuwachanganya akili kabla ya mechi hiyo itakayochezwa majina ya saa 2 usiku kwa hapa kwetu na itaonyeshwa live kupitia mtandao wa Yanga.
Kocha Msidizi wa Yanga, Mkwasa alisema mchezo wa leo utakuwa mgumu kutokana na Yanga kuwafunga wenyeji wao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam na kudai itakuwa kosa kama Yanga itaingia uwanjani na mkakati wa kujihami.
Badala yake kocha huyo alisema Yanga itashambulia huku ikiwa makini kwenye ulinzi, ili kuhakikisha inailiza tena Ahly nyumbani kwao na kuweka rekodi Afrika.
"Naamini hawa jamaa watacheza mchezo wa kutushambulia ili kupata goli la mapema," alisema Mkwasa.
"Tunalifahamu hilo lakini ili kuwapa wakati mgumu ni lazima tumiliki mpira na kuwashambulia muda wote na kutowapa nafasi ya kupanga mashambulizi."
Aidha, Mkwasa alisema katika mikanda ya hivi karibuni waliyoiangalia Al Ahly imeonekana kuwa inatumia zaidi mawinga na mabeki wa pembeni kupiga krosi katika mashambulizi yake lakini wamejipanga kudhibiti mchezo huo.
Mkwasa alisema kila mchezaji wa Yanga yupo kwenye hali nzuri kimchezo na wapo tayari kwa mpambano wa leo.
"Unajua ushindi wa nyumbani umewapa wachezaji hali ya kujiamini," alisema. "Wapo tayari kwa mchezo na kwa kweli kama tutafanikiwa kufanya tulichokipanga kwenye mazoezi yetu, ni wazi tutasonga mbele kwenye mashindano haya."
Akizungumzia kikosi cha leo, Mkwasa alisema kupanga ni kazi ya kocha mkuu, Hans van Pluijm. Hata hivyo alisema hakitabadilika sana kulinganisha na mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita.
Kwenye mchezo huo ambao goli pekee lilifungwa na naodha Nadir Haroub 'Canavaro' kikosi kilichoanza kilikuwa:
Deogratias Munishi 'Dida', Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Canavaro, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi.
Katika mchezo wa leo, Yanga ina anasa ya hata kutofungwa si zaidi ya bao 1-0 na ikasonga mbele angalau kwa njia ya matuta
MICHARAZO MITUPU na watanzania kwa ujumla inaitakia kila la heri Yanga katika mechi hiyo ya leo ili kuweza kufanya vyema na kuwapa furaha mashabiki wa soka ambao wamechoka kuona timu zao zikiwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa.
Yanga ndiyo tiumu pekee ya Tanzania kusalia kwenye michuano hiyo mwaka huu baada ya Azam, KMKM na Chuoni za Zanzibar kung';olewa kwenye mechi ra awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
No comments:
Post a Comment