NJIA nyeupe kwa Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya jioni hii kugawa dozi ya maana kwa Coastal Union, huku watetezi Azam wakilazimishwa na Mbeya City.
Yanga ikiwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam imemfunga mdomo kocha anayechinga sana, Jamhuri Kihwelu 'Julio' baada ya kupata ushindi wa mabao 8-0, huku Amissi Tambwe akifunga mabao manne na kurejea rekodi aliyoiweka msimu uliopita wakati akiwa Simba. Kipigo hicho kimekuja katika Ligi Kuu tangu Yanga ilipoifanyia Kagera Sugar mwaka 1998 ambapo Edibily Lunyamila alifunga pekee yake mabao matano.
Mabao mengi ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Simon Msuva aliyefunga mawili, Salum Telela na Kpah Sherman aliyefunga bao lake la kwanza akiwa na Yanga tangu ajiunge nayo miezi minne iliyopita.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha jumla ya pointi 43 na mabao 36 ya kufunga na kuwaacha Azam kwa pointi sita baada ya watetezi hao kulazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City kwenye uwanja wa Chamazi.
Kwa kufunga mabao manne, Tambwe amefikisha mabao 9 msimu huu katika Ligi Kuu wakati Msuva amezidi kumuacha mbali Didier Kavumbagu wa Azam kwa kufikisha mabao 13 dhidi ya 10 ya mpinzani wake huyo ambaye leo hakushuka dimbani katika pambano la Mbeya City.
No comments:
Post a Comment