STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 22, 2015

HUYU NDIYE KOCHA MKUU MPYA WA SIMBA

SIMBA SC imeingia Mkataba wa miaka mwaka mmoja na kocha Dylan Kerr (pichani) mzaliwa wa Malta na mchezaji wa zamani wa England kwa ajili ya kuinoa klabu hiyo kuanzia Julai 1 mwaka huu. BIN ZUBEIRY inafahamu kocha huyo aliyezaliwa Januari 14 mwaka 1967 mjini Valletta amefikia makubaliano ya kuingia Mkataba wa mwaka mmoja na Simba SC wenye kipengele cha kuongezewa mmoja mwingine, iwapo atafanya kazi nzuri. Uongozi wa Simba SC wakati wote unakiri kuleta kocha Muingereza, lakini umekuwa ukigoma kutaja jina, ingawa BIN ZUBEIRY baada ya uchunguzi wa kina, imefanikiwa kumbaini mwalimu mpya wa Wekundu wa Msimbazi.
DYLAN KERR NI NANI NA AMETOKEA WAPI? Kerr anakuja Simba SC akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Vietnam, Hai Phong aliyojiunga nayo Januari mwaka 2014. Huyo ni beki wa zamani wa kushoto aliyeibukia klabu ya Sheffield Wednesday mwaka 1984. Hakucheza mechi yoyote ya Ligi Kuu katika miaka yake minne ya kuwa na klabu hiyo ya Hillsborough hivyo akahamia Arcadia Shepherds ya Afrika Kusini mwaka 1988. Mwaka mmoja baadaye akarejea England kujiunga na Leeds United, ambako alicheza mechi 13 tu za Ligi Kuu katika miaka yake minne Elland Road kabla ya kutolewa kwa mkopo katika klabu mbili, kwanza Doncaster Rovers alikofunga bao lake la kwanza katika ligi, kisha Blackpool.  Katika miezi yake mitatu ya kuwa na Blackpool msimu wa 1991–1992, alifunga moja ya mabao katika ushindi wa 5-2 ugenini dhidi ya Lancashire na mabingwa wa Daraja, Burnley Uwanja wa Bloomfield Road. Mwaka 1993, Kerr akahamia Mortimer Common kujiunga na Reading, ambako alicheza mechi nyingi zaidi za ligi katika historia yake (89) na kufunga mabao matano.  Alikuwemo kwenye kikosi cha Royals kilichotwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili, na wakati timu hiyo inashika nafasi ya pili katika Daraja la Kwanza msimu uliofuata alikuwepo kikosini. Mwaka 1996, Kerr akasaini Kilmarnock ya Scotland, ambako alicheza mechi 61 za ligi Killie katika miaka minne. Mwishoni mwa msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo, alishinda Kombe la Scotland, kabla ya kuumia nyonga na kuwa nje kwa zaidi ya mwaka.
Dylan Kerr enzi zake anacheza Ligi Kuu England
Mwonekano wa sasa wa kocha Dylan Kerr
Kerr akatemwa Kilmarnock, na baada ya mechi moja ya kucheza kwa mkopo Carlisle United akajiunga na Slough Town Oktoba mwaka 2000, kabla ya Septemba mwaka huo kujiunga kwa muda na Kidderminster Harriers, lakini Mkataba wake wa mwezi mmoja ukasitishwa kwa utovu wa nidhamu. Akarejea Scotland kujiunga na Hamilton Academical Januari mwaka 2001 na miaka mitatu iliyofuata akacheza timu za Exeter City kwa miezi mitatu, Greenock Morton, Harrogate Town, East Stirlingshire na Hamilton Academical kwa mara nyingine kabla ya kustaafu akiwa na Kilwinning Rangers mwaka 2003. Baada ya kutungika daluga zake, Kerr akaenda kufundisha Marekani klabu ya Phoenix, Arizona ambako baada ya kukosa viza ya kuishi nchini humo akalazimika kurejea Scotland, ambako alifanya kazi kama Ofisa Maendeleo wa Argyll na Bute kati ya mwaka 2005 na 2009. Septemba mwaka 2009, Kerr akasaini Mkataba wa kuwa kocha Msaidizi wa Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini hadi Juni mwaka 2010 alipohamia Thanda Royal Zulu kama Kocha Msaidizi pia, 2011 akaenda Nathi Lions (Msaidizi), 2012 akaenda Khatoco Khanh Hoa (Msaidizi) na mwaka 2012 akasaini Mkataba wa kuwa kocha wa mazoezi utimamu wa mwili (feetness) wa timu ya taifa ya Vietnam. Mwaka 2013 akahamia Hai Phong kama Kocha Msaidizi pia, kabla ya mwaka 2013 kuwa Kocha Mkuu wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ya Hai Phong na mwaka 2014 akawa kocha Mkuu wa Hai Phong, ambayo aliipa ubingwa wa Taifa wa nchi hiyo. Kocha huyo kijana, anakuja Simba SC kurithi mikoba ya Mserbia, Goran Kopunovic ambaye baada ya miezi sita ya kufundisha klabu hiyo akashindwana na uongozi juu ya dau la Mkataba mpya. 
Credit:BIn Zubeiry

No comments:

Post a Comment