Watetezi Yanga |
Azam Fc washindi wa pili wa msimu uliopita |
Simba waliokamata nafasi ya tatu msimu uliopita |
Mbeya City iliyokimbiwa na nyota wake wengi |
Michezo saba itakayopigwa kwenye viwanja saba tofauti inatarajiwa kukata utepe wa ligi hiyo, kabla ya keshokutwa Jumapili kupigwa pambano la kukamilisha raundi ya kwanza litakalozikutanisha mabingwa watetezi, Yanga na mabingwa wa zamani Coastal Union ya Tanga.
Mechi za fungua dimba zitakazopigwa leo Jumamosi ni pamoja na lile la mabingwa wa Tanzania wa mwaka 1988 waliorejea Ligi Kuu baada ya miaka zaidi ya 20 itakayovaana na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Simba haijaonja ushindi kwenye Uwanja huo tangu mwaka 2012 pale Patrick Mafisango alipofunga bao pekee na la ushindi wakati timu hiyo ikiizamisha Coastal Union kwa bao 1-0.
Mechi nyingine ni ile itakayozikutanisha Stand United dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, Mwadui itakuwa wageni wa Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na Majimaji Songea itaialika JKT Ruvu katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Ndanda watakuwa wenyeji wa maafande wa Mgambo JKT pale Nangwanda Sijaona, Mtwara, huku Azam itaikaribisha Prisons Mbeya Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na Mbeya City kuvaana na wakata Miwa wa Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Msimu wa 52
Huu utakuwa ni msimu wa 52 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo mnamo mwaka 1965 ikiwa na maana mwaka huu wa 2015 ni mwaka wa 50 tangu kuanza kwa michuano hiyo mikubwa nchini.
Klabu 16, nne zikiwa zilizopanda daraja na kurejea Ligi Kuu ya Bara na nyingine 12 zilizosalimika kwenye ligi iliyopita zitachuana kuwania taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga.
Yanga ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa ligi hiyo tangu mwaka 1965, ikitwaa mara 25, huku wakifuatiwa kwa mbali na watani zao, Simba walionyakua mara 18.
Mtibwa Sugar ya Morogoro ndiyo klabu inayovisogelea vigogo hivyo ikiwa imeshinda ubingwa mara mbili mwaka 1999 na 2000, huku timu nyingine sita za Cosmo, Mseto, Pan Africans, Tukuyu Stars na Azam kila moja zikinyakua mara moja moja na kuhitimisha orodha ya mabingwa wa ligi.
Haina ugeni
Majimaji-Songea, African Sports, Toto Africans na Mwadui Shinyanga ndizo klabu zilizopanda daraja msimu huu zikitokea katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ila ukweli ni kwamba hazina ugeni na ligi hiyo.
Kwa nyakati tofauti timu hizo zimeshaichezea ligi hiyo kabla ya baadhi kuzama kimoja kama ilivyokuwa kwa Mwadui iliyoshuka daraja mwaka 1986, Sports (1991) na Majimaji na Toto Africans zikipanda na kushuka kila zilipokuwa zikijisikia.
Kwa maana hiyo ligi ya msimu huu haina klabu ngeni za ligi hiyo, japo baadhi zimerejea kuichezea ikiwa imepita miaka mingi.
Ujio wa Mwadui na Sports na hata Majimaji unakumbusha enzi za Ligi Daraja la Kwanza ambapo klabu hizo zilijijengea jina kubwa kwa mafanikio iliyopata kwa nyakati tofauti kabla ya kupotea.
Zinakutana na klabu zilizolowea kwenye ligi hiyo kama Yanga, Simba, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Azam na JKT Ruvu ambazo tangu zianze kushiriki ligi hiyo kwa misimu tofauti hazijawahi kushuka daraja.
Mbali na klabu hizo ngangari, pia zitakumbana wakali wengine kama Coastal Union, Prisons-Mbeya, Stand United, Mgambo JKT, Mbeya City na Ndanda.
Mchuano
Kama misimu mingine iliyopita, ligi ya safari hii inatarajiwa kuwa na mchuano mkali kati ya klabu shiriki na hata kwa wachezaji waliosajiliwa na klabu hizo. Inatarajiwa kuwepo kwa mchuano wa wachezaji wazawa na wale wa kigeni (mapro) sambamba na makocha kutunishiana misuli.
Jumla ya makiocha 16 wakuu, wakiwamo sita wa kigeni watakuwa na kazi ya kuthibitisha ubora wao katika msimu huu, sawa na itakavyokuwa kwa wachezaji mapro dhidi ya wazawa ambao msimu uliopita walifunika mwanzo mwisho kwa kunyakua tuzo karibu zote za VPL 2014-2015.
Simon Msuva aliweka rekodi ya kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora akiwa na mabao yake 17 na pia tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu, huku Kipa Bora akiwa ni Shaaban Kado na Kocha Bora ikienda kwa Mbwana Makata.
Je, wazawa wamezinduka na kuendelea kuwafunika mapro au ni nguvu ya soda tu baada ya misimu kadhaa ya kukimbizwa mchakamchaka na wachezaji wa kigeni waliotawala kila kona? Tusubiri, japo inatarajiwa msimu huu inatabiriwa kuibuka kwa nyota wapya ambao watafunika kutokana na vipaji vyao turufu ikiwabeba akina Geofrey Mwashiuya, Matheo Simon, Farid Mussa, Deus Kaseke, Malimi Busungu na wengineo.
Utabiri
Kwa namna klabu zilizofanya usajili mzuri na kufanya maandalizi ya kutosha ni vigumu kutabiri moja kwa moja klabu zenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa msimu huu, lakini kwa kuangalia kikosi kimoja kimoja turufu inaziangukia timu za Yanga, Azam, Simba na Mwadui Shinyanga.
Hata hivyo kwa kuwa soka ni mchezo usiotabirika kirahisi siyo ajabu kuziona Stand United, JKT Ruvu, Majimaji, Coastal Union na Mtibwa Sugar zikichanua na kusumbua msimu huu.
Katika janga la kushuka daraja mwishoni mwa msimu kura inaziangukia Ndanda, Mgambo JKT, African Sports, Toto Africans na Prisons-Mbeya, kama hazitakaza buti na kupambana zitaenda na maji. Hii ni kwa sababu zilionekana kutojipanga kama klabu nyingine, japo siri ya mtungi...!
Zikikaa vibaya zinaweza kujikuta mwishoni mwa msimu zikifuata mkumbo wa Ruvu Shooting na Polisi Moro zilizoshuka msimu uliopita, pia zinapaswa kufahamu msimu huu timu tatu ndizo ambazo zitakazoteremka daraja hivyo zijipange kwelikweli.
Ratiba:
Kesho Jumamosi:
Ndanda v Mgambo JKT
African Sports v Simba
Majimaji v JKT Ruvu
Azam v Prisons
Stand Utd v Mtibwa Sugar
Toto Africans v Mwadui Fc
Mbeya City v Kagera Sugar
Jumapili:
Yanga v Coastal Union
Jumatano:
Yanga v Prisons
Mgambo JKT v Simba
Majimaji v Kagera Sugar
Mbeya City v JKT Ruvu
Stand Utd v Azam
Toto Africans v Mtibwa Sugar
Ndanda v Coastal Union
Alhamisi:
Mwadui FC v African Sports
Orodha ya Mabingwa tangu 1965-20151965- Sunderland (Simba)
1966- Sunderland (Simba)
1967- Cosmopolitan
1968- Yanga
1969- Yanga
1970- Yanga
1971- Yanga
1972- Yanga
1973- Simba
1974- Yanga
1975- Mseto
1976- Simba
1977- Simba
1978- Simba
1979- Simba
1980- Simba
1981- Yanga
1982- Pan Africans
1983- Yanga
1984- Simba
1985- Yanga
1986- Tukuyu Stars
1987- Yanga
1988- Coastal Union
1989- Yanga
1990- Simba
1991- Yanga
1992- Yanga
1993- Yanga
1994- Simba
1995- Simba
1996- Yanga
1997- Yanga
1998- Yanga
1999- Mtibwa Sugar
2000- Mtibwa Sugar
2001- Simba
2002- Yanga
2003- Simba
2004- Simba
2005- Yanga
2006- Yanga
2007- Simba
2007/08- Yanga
2000/09- Yanga
2009/10- Simba
2010/11- Yanga
2011/12- Simba
2012/13- Yanga
2013/14- Azam
2014/15- Yanga
2015/16 ???
Vinara
25-Yanga
18-Simba
2-Mtibwa
1-Cosmo, Mseto, Pan, Tukuyu, Coastal, Azam
No comments:
Post a Comment