KELVIN Yondani ndio basi tena, kwani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya Kusimamia na Kuendesha ligi iliyokutana kwa saa 72 jana Jumatano kupitia taarifa na ripoti
mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu (VPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
zinazoendeea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini imemkuta na hatia.
Taarifa rasmi ya TFF inasomeka hivi:
Ligi Kuu ya Vodacom
Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amefungiwa mechi tatu na kupigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumpiga usoni kwa box la dawa
Dk. Mganga Kitambi wa Coastal Union wakati akitoa huduma kwa kipa wake
katika mechi namba 121 kati ya timu hizo iliyofanyika Januari 30, 2016
kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Yondani alitenda kosa hilo baada ya kumuomba maji Daktari huyo,
lakini akamnyima. Adhabu huyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3)
ya Ligi Kuu Toleo la 2015 ambapo baada ya kutumia adhabu ya mechi hizo,
hataruhusiwa kucheza hadi atakapokuwa amelipa faini hiyo.
Naye Dk. Kitambi anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kitendo
chake cha kumrudishia Yondani kwa kumpiga ngumi. Kitendo cha Daktari
huyo ni kinyume cha Kanuni ya 41(2), na pia Kanuni ya 36 kuhusu mchezo
wa kiungwana.
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu
wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuwatupia chupa za maji
wachezaji wa Coastal Union walipokuwa wakishangilia bao la pili.
Nayo klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano)
kwa washabiki wake kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho, kitendo
ambacho ni kinyume cha Kanuni ya 14(11) inayohusu taratibu za mchezo.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia
chumba cha waandishi wa habari badala ya kile cha timu wakati wa mechi
kati yao na Simba iliyochezwa Februari 3, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14(13)
ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Kocha Ally Jangalu wa Coastal Union ameripotiwa kutoa matamashi ya
kuidhalilisha TFF kwenye vyombo vya habari kuwa Refa wa mechi kati yao
na Ndanda SC iliyochezwa mjini Tanga alikwenda na maelekezo ya
kuhakikisha wapinzani wao wanashinda. Coastal Union ilifungwa bao 1-0
katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2016. Suala lake linapelekwa
Kamati ya Nidhamu.
Mchezaji Daud Jumanne amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) baada ya kumkanyaga vidole kwa makusudi mchezaji wa
Simba aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu kwenye mechi kati ya timu
hizo iliyofanyika Februari 7, 2016 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo
la 2015. Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 37(20), hauruhusiwi kucheza mechi
inayofuata ya timu yake mpaka faini hiyo iwe imelipwa. Iwapo atacheza
kabla ya kulipa faini hiyo, timu yake itapoteza mchezo husika.
Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoingia
vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya African Sports
iliyochezwa Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) kuhusu taratibu za mchezo.
Kamishna wa mechi hiyo namba 140, Idelfonce Magali amepewa karipio
kwa kutoripoti vizuri tukio hilo, wakati Refa Elly Sasii amepewa karipio
kali kwa kutoripoti kabisa tukio hilo.
Ligi ya StarTimes
Wachezaji Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Seleman na Edward Amos wa
Polisi Dodoma wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kumzonga,
kumtolea lugha ya matusi ya nguoni na kutaka kumpiga Refa katika mechi
ya Ligi ya StarTimes kati ya timu yao na African Lyon iliyofanyika
Januari 30, 2016.
Kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini
Dodoma ni kinyume cha Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu
udhibiti wa wachezaji.
Kiongozi wa Friends Rangers, Heri Mzozo anapelekwa Kamati ya Nidhamu
kwa kutoa lugha chafu kwa viongozi na waamuzi muda wote wa mchezo dhidi
ya Ashanti United uliofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Karume
jijini Dar es Salaam. Vitendo vyake ni kiyume na Kanuni ya 41(2) ya Ligi
Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.
Mwamuzi Msaidizi namba 2 kwenye mechi kati ya Kimondo na Ruvu
Shooting, Idd Mikongoti wa Dar es Salaam ameripotiwa na Kamishna
kuondoka na timu ya Ruvu Shooting kwa kupanda basi lao mara baada ya
mchezo, kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya uamuzi. Suala lake
limepelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi kwa ajili ya hatua stahiki dhidi
yake.
Klabu ya Geita Gold imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na
onyo kali kwa kukataa kuingia kwenye chumba cha wachezaj, na badala
yake kutumia chumba kingine ambacho pia walijisadia haja ndogo wakati wa
mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyofanyika Januari 31, 2016 kwenye
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana
na kitendo cha mshabiki wake kupita pembezoni ya uwanja (running track)
kwa kasi wakati mechi hiyo dhidi ya Geita Gold ikiendelea.
Pia klabu ya Polisi Tabora imepewa onyo kali kutokana kipa wa timu
yake kuvaa jezi ambayo haikuwa na nembo (logo) ya Mdhamini wa Ligi
Daraja la Kwanza wakati wa mechi hiyo.
Geita Gold imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya
JKT Oljoro kugomea mchezo kati ya timu hizo uliofanyika Februari 6, 2016
kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls mkoani Geita. Timu hiyo iligomea mechi
hiyo dakika 70 baada ya kufungwa bao la pili. Kitendo hicho ni kinyume
cha Kanuni ya 29(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia JKT Oljoro imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja)
kutokana na kitendo hicho kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4), wakati
wachezaji wake Kapteni Shaibu Nayopa na Sunday Paul waliomvamia na
kumpiga Refa wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa
hatua stahiki.
Naye Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro, Bunu Abdallah ambaye alitolewa
kwenye benchi la timu yake kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mwamuzi
Msaidizi namba 1 anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua
stahiki.
No comments:
Post a Comment