LAZIMA kieleweke. Straika wa kimataifa wa Liverpool, Christian Benteke amesema ni lazima afanye mazungumzo na klabu hiyo kujadili mustakabali wake baada ya kumaliza msimu wake wa kwanza ambao haukuwa mzuri hata kidogo. Benteke amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda klabu kadhaa katika kipindi cha kiangazi ikiwemo West Ham United baada ya kushindwa kung’aa akiwa Anfield akifunga mabao 10 katika mechi 42 za mashindano yote aliyocheza toka anunuliwe kwa kitita cha Pauni Milioni 32.5 kutoka Aston Villa.
Kocha Mkuu wa LIverpool, Jurgen Klopp hakuwa akimpa nafasi kubwa kama aliyokuwa nayo wakati akiichezea Aston Villa, kiasi cha Brendan Rodgers kumsajili kabla ya kutimuliwa baada ya timu kuyumba.
Kukiwa hakuna uwezekano wa kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kufungwa mabao 3-1 na Sevilla katika Fainali ya michuano ya Europa League juzi Jumatano, Benteke amesema yeye sambamba na wachezaji wengine wana matumaini ya kuzungumza na Kocha Klopp kuhusu mipango ya msimu ujao. Akihojiwa Benteke amesema anafahamu kuwa bado anatakiwa kuzoea mazingira na kwasababu msimu umemalizika anadhani sasa ni wakati wa kukaa chini ya Klopp na kujaribu kutafuta suluhisho kwa ajili ya msimu ujao.
Liverpool imemaliza msimu huu wa EPL katika nafasi ya nane ikikusanya pointi 60 katika mechi 38, ikiwa ni pungufu ya pointi 21 na zile za mabingwa Leicester City.
No comments:
Post a Comment