STRIKA
USILIKOSE
Friday, May 20, 2016
YANGA YATUA KIBABE, ILA INA KAZI NGUMU
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania na Ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Yanga mchana huu wametua jijini Dar es Salaam kutoka Angola walikoenda kuweka rekodi Afrika kwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Yanga iliikubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya wenyeji wao GD Segrada Esperanca ya Angola, lakini hazina ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoshinda katika mechi yao ya awali nyumbani jijini Dar es Salaam iliwavusha kwa jumla ya mabao 2-1.
Mashujaa hao wa Tanzania walitua saa 8 mchana na kupokewa na umati mkubwa wa mashabiki, huku Kocha Hans Pluijm akiwapongeza vijana wake kupambana kiume ugenini na hatimaye kupenya.
ILIVYO SASA
Kwa sasa Yanga na mashabiki wao na wadau wachache wa soka ambao uweka mbali ushabiki wao na kuvaa joho la uzalendo, wanashangilia mafanikio hayo ya Yanga kwani ni heshima kwa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Achana na kitita cha fedha ambacho Yanga kitavuna kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya makundi, lakini vijana hao wa Jangwani wamepata nafasi nyingine ya kufukia mashimo yote ya nyuma.
Kama hujui ni kwamba Yanga itapewa kiasi cha dola 150, 000 (zaidi ya Sh. 300 Milioni) kwa kufuzu hatua hiyo, huku ikiipa Shirikisho ya Soka (TFF) dola 15,000 (zaidi ya Sh. 30 Milioni 30).
Lakini dau hilo litapanda zaidi kwa Yanga hadi kufikia adi dola 239,000 (Sh. 500 Milioni) na TFF kuvuna dola 20,000 (zaidi ya 40 Milioni, iwapo itamaliza nafasi ya tatu katika kundi itakalopangwa.
Yanga ikiingia fainali itapata dola 432,000( Sh. 879 Milioni) TFF ikivuna dola 30,000 na kama itatwaa ubingwa basi Yanga itapewa dola 625, 000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.2, wakati TFF itapata dola 35, 000 (Sh. Milioni 700).
PEKE YAO
Yanga ndio wawakilishi hao wa pekee wa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) imeweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ikiwekwa mikononi mwa Waarabu.
Yanga imeweka rekodi hiyo ikiwa ni miaka 18 tangu ilipoweka rekodi nyingine ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 kabla ya watani zao Simba kufuata nyayo zao mwaka 2003.
Hata hivyo ushiriki wake wa hatua kama hiyo katika Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 ulikuwa wa aibu, ikizingatiwa Simba ilipotinga hatua kama hiyo miaka mitano baadaye ilitakata na kuifunika Yanga, hata kama haikuvuka kutinga nusu fainali.
LIGI YA MABINGWA
Yanga katika safari yake ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza mwaka 1998, haikuwa na kibarua kigumu kwani ilianza kuumana na Rayon Sports ya Rwanda katika raundi ya kwanza.
Yanga ilianzia ugenini kwa kulazimisha sare ya mabao 2-2 kabla ya kupata nyingine ya bao 1-1 nyumbani na kutinga raundi ya pili ambapo walipangiwa na Coffee Ethiopia walioing'oa kibabe kwa jumla ya mabao 8-3.
Yanga ililazimishwa sare ya 2-2 ugenini kabla ya kushinda nyumbani kwa mabao 6-1 na hatimaye kutinga kwenye makundi ambapo hata hivyo kocha aliyeisaidia timu hiyo kutinga hapo, Tito Mwaluvanda alifurushwa na timu kupewa Raoul Shungu.
MAKUNDI
Katika makundi, Yanga iliwekwa kundi B na timu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast waliokuja kuwa mabingwa, Mining Rangers ya Afrika Kusini na Raja Casablanca ya Morocco.
Ilianza kwa sare ya 1-1 na Maning Rangers kabla ya kwenda kukandikwa mabao 6-0 na Raja kisha kupokea kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Asec na waliporudiana nao Waivory walishinda mabao 3-0 jijini Dar es Salaam.
Yanga iliendelea kutoa takrima kwa wapinzani wake kwa kunyukwa mabao 4-0 huko Afrika Kusini na Mining na kuja kutoka sare ya mabao 3-3 na Raja. Mwishowe Yanga ilimaliza mkiani ikiwa na pointi mbili tu, ikiwa timu iliyofungwa mabao mengi(19) na kufunga machache (5) na kuziacha Asec na Mining zikisonga mbele kwa nusu fainali.
SIMBA YAFUNIKA
Baada ya timu za Tanzania kusota kwa miaka mitano, Simba ilifuata nyayo za Yanga mwaka 2003 kwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa tena kwa kuivua ubingwa, watetezi Zamalek ya Misri kwa mikwaju ya penalti.
Matokeo ya mwisho yalisomeka bao 1-1 kwani kila timu ilishinda mchezo wa nyumbani na Simba wakafanya kweli kwenye mikwaju ya penalti na kutinga makundi.
Tofauti na Yanga, Simba ilionyesha uhai kwelikweli kwa kushinda mechi mbili na kuambulia sare moja na kumaliza nafasi ya tatu ikiziacha timu zilizofuzu kucheza fainali Asec Mimosas na Ismailia ya Misri zikionyeshana ubabe mwishoni.
Simba ilianzia ugenini na kukandikwa mabao 3-0 na Enyimba kabla ya kuja kuituliza Asec jijini Dar kwa bao 1-0 na kuidindia Ismailia kwa sare isiyo na mabao na walipoenda Misri kurudiana na wapinzani hao hao walikubali kipigo cha 2-1.
Waliporudi nyumbani waliikaribisha Enyimba kwa kipigo cha mabao 2-1 na kwenda kupoteza ugenini kwa mabao 4-3 dhidi ya Asec na kujikuta ikimaliza nafasi ya tatu ikiwa ni timu ya pili iliyofungwa mabao machache (10) nyuma ya Ismailia (7).
MIAKA YA MATESO
Tangu Simba na Yanga ziliposhiriki hatua ya makundi Afrika, klabu hizo na wawakilishi wengine wa Tanzania walikuwa kama watalii tu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho hadi mwaka huu Yanga ilipofanya kweli.
Yanga ilianzia michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kuing'oa Cercle de Joachim ya Mauritius katika raundi ya awali kisha kuiondosha APR ya Rwanda katika raundi ya kwanza na kupangiwa wababe wa Misrim, Al Ahly iliyowatupa nje kwa mabao 3-2.
Ndipo ikakutana uso kwa uso na GDS Esperanca ya Angola na kuwafunga mabao 2-1.
Pamoja na kusaka fedha zinazotolewa kwa klabu zinazocheza hatua ya Nane Bora, bado Yanga inapaswa kupambana kuweza kuweka heshima na kufunika ikiwezekana mafanikio ya watani zao Simba mwaka 2003.
Hakuna ubishi Yanga haina rekodi ya kujivunia katika michuano ya Afrika ukiondoa mara tatu zilizocheza robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (1969 na 1970) na Kombe la Washindi mwaka 1995.
WAARABU TENA
Yanga imekuwa na gundu dhidi ya timu za Kiarabu na katika klabu nane zilizotinga hatua hiyo ya makundi kabla ya ratiba na makundi mawili kupangwa Jumanne ijayo (mei 24), lazima iwe mikononi mwa klabu hizo za Afrika Kaskazini.
Klabu tano za Waarabu zilizopenya ni MO Béjaïa (Algeria), Al Ahli Tripoli (Libya), FUS Rabat na Kawkab Marrakech (zote za Morocco) na Etoile du Sahel (Tunisia) ambazo zimeungana na Yanga, TP Mazembe ya DR Congo na Medeama ya Ghana.
Ikiwa na kikosi imara chenye kuundwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu kisoka, huku wakiwa na Kocha mjanja, Hans Pluijm na wasaidizi wake, Juma Mwambusi na Juma Pondamali, Yanga inaweza kufanya mambo kama ikiamua.
HESABU KALI
Lazima ipigie hesabu mechi zake za nyumbani, ili kujitengenezea mazingira ya kushika nafasi mbili za juu za kutinga nusu fainali na kuogelea kwenye mamilioni ya fedha za CAF, hata wenzao hutumia mechi za nyumbani kujinufaisha nao wasizubae.
Yanga isijiamini kupita kiasi na kuzichukulia poa timu itakazocheza nao kwa sababu ya mafanikio iliyopata kwa hivi karibuni, itambue kuwa kazi ndio kwanza imeanza.
Ni nafasi kwa kina Deus Kaseke, Simon Msuva, Mwinyi Haji, Deo Munishi, Ally Mustafa, Juma Abdul, Paul Nonga, Matheo Simon na wengine wakiwamo wageni kujiuza kupitia michuano hiyo, sambamba na kurejesha heshima ya Yanga kimataifa.
MICHARAZO MITUPU inawatakia kila la heri katika kufanikisha mipango yao ya kujenga heshima Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment