RAHMA WHITE
WAKATI mashabiki wa soka nchini na Afrika Mashariki wakihesabu saa zilizosalia kabla ya kitendawili cha nani mbabe kati ya wapinzani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga hazijakutana jioni ya leo Jumapili hii katika pambano la Ligi Kuu, winga matata waSimba, Shiza Kichuya yupo katika nafasi nzuri ya kuandikisha rekodi tamu.
Kichuya anayeichezea Simba kwa msimu wa pili sasa tangu alipotua Msimbazi akitokea Mtibwa Sugar na kuifungia jumla ya mabao 19 katika Ligi Kuu, ni kati ya nyota watatu wanaoshikilia rekodi ya kufunga kwenye mechi tatu mfululizo wa watani.
Winga huyo anakula sahani moja na nyota wa zamani wa Simba, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' na straika wa Yanga, Amissi Tambwe, lakini kuwepo kwa mchezo wa Jumapili unampa nafasi mkali huyo kuwapiku wenzake na kuandika rekodi tamu.
Kama Kichuya atafanikiwa kuivuruga tena ngome ya Yanga na kufunga bao, atakuwa ndiye kinara na hivyo kuwapiku Madaraka aliyestaafu soka muda mrefu na Tambwe ambaye msimu huu amekuwa na wakati mgumu kuwa majeruhi wa muda mrefu.
Kichuya aliwafikia Mzee wa Kiminyio na Tambwe kwa mechi tatu zilizopita za watani ikiwamo ile ya kwanza kwanza akiwa na uzi wa Simba iliyopigwa Oktoba 1, 2016 akichomoa bao la Yanga liliwekwa na Tambwe na kusababisha vurugu za mashabiki.
Bao lake la pili alilitupia alipoisaidia Simba kuitungua Yanga katika mechi yao ya Februari 16 mwaka jana wakati Msimbazi wakiitambia Jangwani kwa mabao 2-1. Bao jingine la Simba lililokuwa la ushindi likiwekwa wavuni na Laudit Mavugo.
Katika mechi ya mwisho ya watani hao kukutana Oktoba 28, pia mwaka jana ikiwa mchezo wa duru la kwanza, Kichuya tena alifanya mambo ya kuitanguliza Simba kwa bao la dakika ya 57 kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika tatu baadaye.
Kwa mazingira yaliyopo kwa winga huyo ni nafasi yake ya kuandika rekodi hiyo mpya kama ambavyo nyota wenzake, John Bocco na Emmanuel Okwi walivyo na kibarua cha kuvunja rekodi ya hat trick ya mechi ya watani inayoshikiliwa na Abdallah Kibadeni.
King Kibadeni aliandikisha rekodi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 40 sasa katika pambano la kihistoria la watani lililopigwa Julai 19, 1977 wakati Simba ikiitambia Yanga kwa mabao 6-0, huku yeye akifunga matatu na mengine mawili yakiwekwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' na beki wa Yanga Selemani Sanga alijifunga.
Pambano hilo la watani ambalo litakuwa la 100 tangu klabu hizo kongwe zianze kukutana katika mechi za Ligi ya Bara, inasubiri kuona rekodi mbalimbali zikivunjwa ikiwamo ya matokeo ya kipigo kikubwa ama sare ya maajabu zilizowahi kuwekwa 1996 na 2003 timu hizo zilipofungana mabao 4-4 na 3-3 mtawalia bila kutarajiwa.
No comments:
Post a Comment