STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 23, 2010

Mama Sitti Mwinyi ataka uchaguzi wenye amani na salama



WAKATI kampeni za wagombea wanaowania kinyang'anyiro cha uchaguzi zikiendelea nchini kote, Mke wa Rais wa Pili Mstaafu, Ally Hassani Mwinyi, Sitti Mwinyi, ameibuka na kuuombea uchaguzi huo uwe wa salama na amani.
Pia aliwahimiza wanawake nchini kote kuchangamkia uchaguzi huo kwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuhakikisha wanawachagua viongozi watakaosaidia kudumisha umoja na mshikamano.
Mama Sitti alitoa wito huo alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ofisi mpya ya Taasisi ya Kijamii ya Al Madinah, iliyoambatana na ufuturishwaji wa futari kwa wanawake wa Kiislam uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, wananchi bila kujali itikadi ya kidini au siasa wahakikishe kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa amani na utulivu wakiwa na maelewano kwa lengo la kudumisha umoja na mshikamano kwa watanzania wote.
"Nawasihi wananchi wote wake kwa waume bila kujali dini, kabila au itikadi za kisiasa washiriki uchaguzi mkuu kwa amani na salama wakiwa na maelewano, ili kudumisha umoja wetu," alisema.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na mke mkubwa wa Mwinyi, Bi Khadija, alihudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Wanawake wa Al Madinah inayoongozwa na Hajat Mariam Dedesi na kudhaminiwa na Benki ya Stanbic.
Bi Khadija, alisema kwa kuwa Tanzania ni moja na wananchi ni wamoja ni vema wakashirikiana kuona uchaguzi wao unafanyika kwa amani na utulivu ili kuendeleza hali hiyo iliyozoeleka nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Wanawake ya Al Madinah, Mariam Dedesi alisema lengo la kuandaa futari hiyo kwa wanawake wenzao ni kujenga umoja na mshikamano na pia kusaidia kuhamasisha wenzao kujiunga na benki kwa lengo la kujiwezesha na hasa benki zisizo na riba.
Alisema kamati yao inawahamasisha wanawake kujiunga na mabenki yasiyo na riba ili kuweza kukopa fedha za kujianzishia miradi ya kimaendeleo ambazo itawakwamua kiuchumi wao na familia zao.

Mwisho

No comments:

Post a Comment