STRIKA
USILIKOSE
Monday, August 23, 2010
Waislam wahimizwa kujiunga na benki zisizotoza riba
WAUMINI wa dini ya Kiislam wamehimizwa kujiunga na mabenki kwa lengo la kuhifadhi fedha zao kwa salama pamoja na kuwawezesha kupata fursa ya kukopa fedha za kuendeshea shughuli zao za kimaendeleo na uchumi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kidini na Kijamii ya Al Madinah, Sheikh Ally Mbaraka, alipozungumza na Micharazo mara baada ya uzinduzi wa ofisi yao mpya eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Mbaraka alisema ni vema waumini wa Kiislam wakajiunga na mabenki na hasa yasiyotoa riba kwa lengo la kupata fursa ya kukopa fedha ili kuanzisha miradi ya kimaendeleo na kiuchumi kujikwamua kimaisha.
Alisema kutokana na kujitokeza kwa mabenki kadhaa yanayoendesha shughuli zao kwa kuzingatia Sharia za Kiislam ni wasaa nzuri kwa waumini kujiunga nazo kuzilinda fedha zao salama na pia kupata faida bila kumuasi Mola wao.
Aliongeza kuwa taasisi yao inayohusika na masuala ya huduma za kijamii na kuratibu safari za Mahujaji, inawaomba waumini wanaotarajia kwenda Hija kuchangamka kujitokeza mapema kujiandikisha kwenye ofisi zao.
"Safari za Hija zinakaribia kuanza hivyo tunawahimiza waumini watakaoenda kuhiji kujitokeza mapema kujiandikisha ili kuwahi nafasi chini ya taasisi yetu ambayo inaendesha shughuli zake kwa kushirikiana na benki ya Stanbic itakayowawezesha mahujaji kutoa na kutuma fedha wakiwa hija," alisema.
Naye Meneja wa Huduma wa Benki ya Stanbic, Jennifer Hillal, alisema benki yao imeweka huduma mbalimbali zinazozingatia sharia ya kiislam kwa lengo la kuwawezesha watu wa imani hiyo kujiunga nao ili wanufaike na mikopo isiyo na riba pamoja na kusaidia kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Alisema benki yako yenye huduma ya ATM Visa Card ni muhimu kwa mahujaji kujiunga nayo kwa vile popote watakapokuwepo hata huko kwenye hija zao wataweza kupata huduma za kifedha kwa mfumo ule ule.
Pamoja na kuwahimiza kujiunga nao, pia aliwataka waumini hao na wananchi kwa ujumla kuingia kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31 wakihakikisha unakuwa wa amani na utulivu.
Jennifer, alisema bila ya kuwepo kwa amani na utulivu hata wao wenye mabenki na watanzania kwa ujumla hawawezi kuendesha shughuli zao za kimaendeleo na kiuchumi kama inavyoshuhudiwa na mataifa mengine.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment