STRIKA
USILIKOSE
Tuesday, August 3, 2010
Phiri awatuliza Simba, atua na kuomba radhi * Aahidi ushindi Agosti 14
KOCHA mkuu wa Simba, Patrick Phiri, alirejea nchini jana mchana kwa ajili ya kuendelea na kibarua chake cha kuwafundisha mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara na akawaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kuchelewa kujiunga na timu.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Phiri alisema kuwa matatizo ya kifamilia yaliyokuwa yanamkabili ndio yalifanya achelewe kuripoti kambini na anaahidi kwamba hatarajii jambo hilo tena.
Phiri alisema kuwa haikuwa rahisi kwa yeye kuondoka na kuiacha familia yake bila ya kutatua matatizo aliyokuwa nayo (hakuyaweka wazi) na kwamba kwa muda wote alikuwa akiwafahamisha viongozi wa Simba kuhusu maendeleo yake.
"Najua kwamba nimechelewa, nawaomba mnisamehe, nitatumia muda uliobakia kuinoa timu ili ifanye vizuri katika Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa mapema mwakani," alisema kocha huyo ambaye alilakiwa na baadhi ya wanachama kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema kuwa pamoja na kuchelewa lakini pambano dhidi ya watani zao, anaamini watashinda kwa vile timu yao ni nzuri kuliko watani zao.
Simba na Yanga zinatarajiwa kupepetana kwenye pambano la Ngao za Hisani kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mechi itakayochezwa Agosti 14.
Phiri aliondoka jijini Dar es Salaam na kuelekea Zanzibar kuungana na timu ambayo imeweka kambi tangu wiki iliyopita ikiwa chini ya makocha Syllersaid Mziray, Suleiman Matola na Amri Said.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' aliliambia gazeti hili kwamba mkataba wa kocha huyo umebakiza miezi michache na baada ya kumalizika uongozi utafanya upya mazungumzo naye kabla ya kuongeza mkataba mwingine.
Simba iliyopangwa kuanza ligi kwa kucheza na African Lyon, itacheza mechi ya kirafiki na Express ya Uganda Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment