TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Wilaya ya Kilosa, imeanza makali yake kwa kuwafikisha mahakamani baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa na ubadhilifu wa fedha za halmashauri hiyo.
Kaimu Kamanda wa Takukuru wilayani humo, Heri Mwankusye, aliiambia Micharazo mjini humo kuwa, tangu ofisi yao ifanyiwe mabadiliko ya kupelekwa watendaji wapya, wameweza kufungua jumla ya kesi tano ambazo watuhumiwa wake wamefikishwa mahakamani.
Mwankusye alisema kesi hizo ni za kuanzia kipindi cha Januari na Desemba mwaka huu, ambapo moja inawahusisha watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Kilosa, ambayo ilifunguliwa mwezi uliopita ikihusisha utafunwaji wa Sh. Mil. 3.7.
Katika kesi hiyo inamhusisha pia karani wa benki ya NMB wilayani humo pamoja na maafisa wengine wakuu wa halmashauri hiyo (idadi na majina yao tunayo).
Mwankusye alizitaja kesi zingine ni ile inayomhusisha Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbumi, aliyestakiwa kwa kosa la kupokea hongo ya Sh 5,000 ambapo kesi yake ipo hatua ya mwisho kabla ya kutolewa hukumu.
"Kesi hii ipo hatua ya mwisho na hukumu yake itatolewa Desemba 17 mwaka huu, kesi nyingi ni ile inayomhusu Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo yta Msowelo, anayeshtakiwa kwa kupokea rushwa ya Sh 60,000," alisema.
Kamanda huyo alizitaja kesi zingine kuwa ni ile ya Afisa Mifugo wa Kata ya Kisanga aliyeshtakiwa pamoja na askari kwa tuhuma za rushwa ya Ng'ombe nane na fedha taslim, Sh.Mil. 1, huku kesi ya mwisho ikiwa inahusisha askari wawili, nao wakidaiwa kupokea rushwa ya ng'ombe katika kata hiyo hiyo ya Kisanga.
Mwankusye alisema kesi hizo ni mwanzo wa taasisi yao kushughulikia tuhuma zinazowasilishwa kwao kila kukicha juu ya kuwepo kwa ubadhilifu na vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwa watendaji wa halmashauri hiyo ya Kilosa.
"Huu ni mwanzo wa kasi yetu ya kushughulikia vitendo vya rushwa na ubadhilifu, lengo ni kutaka kuthibitishia umma kwamba tupo kazini na hasa baada ya Rais kutupa meno," alisema Mwankusye.
Alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano kuweza kuwashughulikia watendaji hao na kuisaidia serikali katika kupambana na kukomesha vitendo hivyo vinavyochangia kurudisha maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mwisho
No comments:
Post a Comment