STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 6, 2010

Wahanga wa Kilosa waulalamika kutelekezwa







WAHANGA wa Mafuriko ya Kilosa, wanaoishi kwenye Kambi ya Mazulia wilayani humo, wameulalamikia uongozi wa wilaya hiyo kwa kuwatelekeza bila msaada wowote, huku vyakula vyao vya misaada vikiharibika na kutupwa na vingine kuchomwa moto jalalani.
Pia wahanga hao wamedai hadi sasa hawajui hatma yao ndani ya kambi hizo zilizopo Kata ya Magomeni, kutokana na mara kwa mara kupokea vitisho vya kuhamishwa vinavyotolewa na watendaji wa wilaya hiyo wanaodai wanatumwa na Mkuu wao wa wilaya, Halima Dendegu.
Wakizungumza na Micharazo kwenye kambi hizo, iliyopo Kata ya Magomeni, wahanga hao walidai uongozi wa wilaya hiyo umewatelekeza bila kuwapa misaada iliyotolewa na wasamaria wema na badala yake vyakula na misaada hiyo ikiharibika na kutupwa au kuchomwa moto.
Wakazi hao walisema mara ya mwisho kupelekewa misaada ilikuwa ni Mwezi Machi na kwa mujibu wa makubaliano ya awali ni kwamba wangekuwa wakipewa misaada hiyo kila baada ya miezi mitatu vitu ambavyo havikufanyika.
Walisema misaada ya mwezi Juni hawakupewa kwa maelezo ya kwamba walilimiwa mashamba na uongozi wa serikali ya wilaya, ambayo walidai hayakutoa mavuno ya kutosha kwa vile yalilimwa wakati mbaya na cha ajabu tangu hapo hawajapewa tena.
"Hatujapewa misaada tangu Machi na hivi karibuni baadhi ya misaada yetu kama nguo na chakula vilienda kutupwa eneo la Ilonga kutokana na kuharibika na Novemba 18 vyakula vyetu vilichomwa moto kwa maelezo vimeharibika, hii ni haki kweli?" alihoji Peter Thomas, 68.
Thomas, alisema hata pale wanapojaribu kuulizia sababu ya kufanyiwa ukatili huo kana kwamba wamependa kuishi kambini hapo, wamekuwa wakipokea vitisho ikiwemo watu walioenda kwao kama Tume maalum ya kuhakiki kambi hiyo waliowaeleza karibia watahamishwa warejee makwao.
"Yaani kwa kifupi tumekuwa tukiishi kwa mashaka bila kujua hatma yetu ndani ya kambi hii, misaada yetu inayeyuka na kibaya tunatishwa tukiambiwa tulikuwa tukibembelezwa kwa sababu ya uchaguzi tu, na sasa uchaguzi umeisha tutalijua jiji," alisema Thomas.
Naye Verena Philipo Mcharo, alisema hivi karibuni mkuu wao wa wilaya aliwapelekea msaada wa mabati sita, mbao moja, misumari kilo moja na mfuko mmoja wa saruji kwa wale waliobomokewa na nyumba zao ili kwenda kujenga katika viwanja walivyopewa bila kujua vilipo.
"Ebu fikiria vifaa hivyo vitatosha nini kama sio kutaka kuwadhihaki watu, tena sio wote waliopewa hati za viwanja walivyoelezwa wametengewa kwenda kujenga makazi yao mapya na sisi tuliokuwa wapangaji tumeambiwa tujue la kufanya kwani misaada hiyo haituhusu," alisema.
Verana, alisema yeye alipohoji kubaguliwa huko miongoni mwa wahanga wa janga hilo la Mafuriko lililotokea mwishoni mwa mwaka jana, aliambiwa anapaswa kurejea kwao Iringa, bila kujali kama alikuja Kilosa kama raia mwingine kwa ajili ya kutafuta maisha.
Mwenyekiti wa kambi hiyo, Msagati, alisema kwa kifupi ni kwamba wao hawajui hatma yao ndani ya kambi hiyo kutokana na mambo yanavyoendelea, huku akitaka waonyeshwe viwanja walivyopewa hati ya kuvimiliki wajue cha kufanya ili kuondokana na dhiki wazipatazo.
Naye Tabia Athuman Matiangu, 71, alidai Septemba 20, mwaka huu alipigwa kofi na Mkuu wa Wilaya kwa kile kilichoelezwa kuwa na kiherehere cha kuwasemea wenzake wakati wa ukaguzi wa wahanga kambini hapo.
Madai ya ajuza huyo, yalithibitishwa pia na baadhi ya wahanga hao, wakidai lilifanyika kama moja ya vitisho dhidi ya malalamiko yao kwa uongozi huo wa wilaya.
Micharazo iliwasiliana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Dendegu, aliyekuwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam, kwa njia ya simu ambapo alikiri kusikia malalamiko hayo, ila alisema ni 'mtandao' maalum ulioundwa kumchafua kutokana na msimamo wake wa kuwakomalia watendaji wa halmashauri hiyo.
"Madai ya wananchi hao hata mie yamenifikia, lakini mengi ni yenye nia ya kutaka kunichafua na yanafanywa na watu wa halmashauri kutokana na madudu yao yaliyofanya hadi wilaya hii ipewe hati chafu kwa upotevu wa fedha kibao za miradi ya maendeleo," alisema Dendegu.
Alikiri kuchomwa kwa vyakula, bila kufananua kiwango chake na sababu zilizofanya kufanywa kwa kitendo hicho kwa madai yupo nje ya ofisi na hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila kitu na kumuomba mwandishi huyu aonane nae baada ya kurejea ofisini kitu kilichoshindikana.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi zilizopatikana ndani ya wilaya hiyo chakula kilichoharibika na kuchomwa moto vikijumuisha Maharage, Ngano, Mchele na Unga wa Sembe ni karibu tani mbili (kilo 1,700).
Alipoulizwa juu ya dai la kumpiga kofi mmoja wa wahanga hao, Mkuu huyo, alionyesha mshangao na kukanusha, huku akihoji mambo hayo yameibukia wapi kipindi hiki ambacho ofisi yake inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wahanga hao.
Juu ya mgao wa vifaa vya ujenzi kwa wahanga hao, alisema ni kweli alitoa mgao huo kiduchu kutokana na jinsi msaada wenyewe ulivyoletwa kwenye ofisi yake.
"Ni kweli niliwapa vifaa hivyo kama walivyokuambia, ila vinaonmekana vichache kwa sababu ndivyo vilivyolewa na wasamaria wema, hatuna mahali pa kuhifadhia hivyo tumewapa wahifadhi wenyewe wakati tunasubiri vingine," alisema.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema, anaamini wanaeneza taarifa hizo kwa kutumia vyombo vya habari wana nia ya kumchafua mbele ya umma, ila alisisitiza hatishiki kwa vile tangu aanze kuaminiwa na serikali na kuteuliwa hajawahi kuharibu mahali popote.

Mwisho

No comments:

Post a Comment