STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 6, 2010

CCM Kilosa waambiana kweli, wapashana kuacha majungu




UONGOZI wa Chama cha Mapinduzi, CCM, Wilaya ya Kilosa, umewataka wanachama wake waache majungu na mifarakano na badala yake washikamane kukijenga chama chao pamoja na kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi walioshinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Viongozi wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Christopher Wegga na Katibu wake, Gervas Makoye walitoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati wa mapokezi na sherehe ya kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi zilizofanyika wilayani humo.
Makoye, aliyehutubia katika mkutano wa mapokezi ya Mkulo, yaliyofanyika kwenye uwanja wa CCM wilayani hapo, alisema kwa kuwa uchaguzi mkuu umeshamalizika ni vema wanachama wa chama hicho wakazika tofauti zao na kushirikiana na walioshinda kukijenga chama chao.
Katibu huyo, alisema pamoja na uchaguzi huo kumalizika na chama chao kuzoa ushindi wa kishindo, bado wapo baadhi ya wanachama wanaendeleza majungu na maneno kitu alichodai haisaidii.
Alisema wanaofanya hivyo ni wanachama waliozoea kupiga mizinga (kuomba hela) na kuwataka wenye tabia hiyo kubadilika kwa sababu chama hakitawavumilia.
"Wanachama wa CCM na wana Kilosa kwa ujumla acheni kupiga maneno, acheni majungu tushikamane kukijenga chama, tuwape ushirikiano wa kutosha viongozi walioshinda kwa sababu uchaguzi umeisha na hivyo tunapaswa kuvunja kambi zetu tuwe kitu kimoja," alisema.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Christopher Wegga, akihutubia kwenye hafla ya kupongeza Waziri Mkulo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Babylon, alisema kuendeleza majungu na tofauti baada ya uchaguzi ni kukwaza maendeleo ya wilaya yao na kuwataka wananchi kushirikiana.
Alisema binafsi anampongeza Waziri Mkulo kwa kurejeshwa kwenye cheo chake cha uwaziri na kuwapongeza wazee walioandaa sherehe hiyo.
Sherehe hiyo ya kumpongeza Mkulo, iliandaliwa na Baraza la Wazee wa Kilosa, ambapo Mwenyekiti wake, Raphael Chayeka, alisema wamefurahishwa mno na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumrejesha Mbunge wao kwenye nafasi hiyo kwa imani Kilosa itapata maendeleo zaidi.
"Imani yetu ni kwamba cheo ulichopewa ni fahari kwetu wana Kilosa, wewe ni kama Rais wetu na tunaamini Kilosa itasonga mbele, tunakutakia kila la heri mna mafanikio," alisema Chayeka.
Waziri Mkulo, aliwashukuru wazee hao, wanachama na wananchi wa Kilosa kwa ujumla kwa kuonyesha imani yake kwake na kuwaahidi kuwasaidia kuwaletea maendeleo ili miaka mitano ijayo Jimbo hilo libadilike na litofautiane kuliko miaka mitano iliyopita.
Ila alisema jambo la muhimu ni wananchi bila kujali itikadi za vyama, dini, jinsia, kabila kushirikiana pamoja katika kupigania wilaya yao iondokane na vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo yao.
****



Na Badru Kimwaga, Aliyekuwa Kilosa
WAZIRI wa Fedha na Uchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amesema pamoja na kuwasamehe wale wote waliompakazia mabaya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, bado hawezi kuwasahau hadi anaingia kaburini.
Pia, amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Kilosa kwa ujumla, kuzika tofauti zao zilizosababishwa mchakato wa uchaguzi mkuu, ili kuweza kushikamana kuijenga wilaya na jimbo lao la Kilosa liweze kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Akizungumza kwenye mapokezi na hafla ya kupongezwa kuteuliwa tena kuwa waziri, Waziri Mkulo, alisema kashfa alizokuwa akipewa akidaiwa sio raia wa Tanzania na kejeli zingine ni vitu ambavyo vilimuumiza, ila amewasamehe wote waliomfanyia jambo hilo.
Waziri alisema hata hivyo pamoja na kuwasamehe wahusika, katu hatawasahau kwa vile walimpa wakati mgumu na kumnyima raha, kitu alichodai kitaendelea kubaki kichwani mwake hadi kifo.
Alisema wale walioanzisha na kueneza maneno hayo na waliomtusi, wasimuogope kwa sababu anafahamu siasa ni mchezo usio na simile na wenye kuhitaji uvumilivu mkubwa kitu alichoweza kukimudu na ndio maana amewasamehe kwa yote.
"Walionitusi na kunizushia kwamba mie sio raia na wengine kufikia hata kumhusisha mke wangu, wote nimewasamehe, ila kwa hakika sintowasahau, muhimu nataka kuwaambia wahusika wasiwe na hofu juu yangu yale yamepita kwani najua siasa ndivyo zilivyo," alisema Mkulo.
Alisema kama sio mambo ya siasa, kwa hakika angeweza kuwafungulia mashtaka na kudai fidia kubwa wahusika wote waliomchafua kipindi cha kura za maoni ndani ya CCM na hata kwenye uchaguzi mkuu uliompa ushindi wa kishindo yeye Mkulo na chama chake.
Waziri Mkulo, alisema kwa kuwa uchaguzi umeshapita kwa sasa yeye ni mbunge wa wakazi wote wa Jimbo la Kilosa na hivyo atawatumikia wananchi wote kwa ajili ya kuwaletea maendeleo, akiomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha aliyopanga kwa miaka mitano ijayo.
Wakati wa mchakato wa kura za maoni, Waziri Mkulo alivumishiwa kuwa yeye si raia wa Tanzania na kikundi cha watu waliojiita Wazee wa Kilosa, ambao walikuja kurukwa na uongozi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo waliodai hawakumtuma mhusika aliyeanzisha chokochoko hizo.
Pia baada ya kushinda kiti hicho cha Ubunge kwa mara ya pili, baadhi ya watu walidaiwa kuapa kuwa asingekuwa miongoni mwa wateule wa Baraza Jipya la Mawaziri, kitu kilichoenda kinyume kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumtangaza kuendelea kushikilia wizara hiyo ya Fedha.

Mwisho
Mwisho

No comments:

Post a Comment