KUNDI la Mapacha Watatu linaloundwa na waimbaji mahiri nchini, Khalid Chokoraa, Jose Mara na Kalala Junior wanatarajia kuonyeshana kazi na msanii anayekuja juu katika miondoko ya muziki wa kizazi kipya Sam wa Ukweli.
Mapacha hao watatu na Sam wa Ukweli watakutanishwa kwenye onyesho la pamoja lifahamikalo kama 'Usiku wa Sauti za Kizazi Kipya cha Dansi' litakalofanyika Desemba 13, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa onyesho hilo, Sauda Mwilima, aliiambia Micharazo kuwa, onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Stereo Bar, Kinondoni na wasanii hao wataonyesha umahiri wao.
Mwilima alisema onyesho hilo linawagusa Mapacha Watatu, watakaofanya vitu vyao kwa kutoa burudani na watasindikizwa na msanii Salum Mohamed 'Sam wa Ukweli' anayetamba na ngoma yake iitwayo 'Sina Raha'.
"Usiku wa Sauti ya Kizazi Kipya cha Dansi utaporomoshwa na Mapacha Watatu, wakisindikizwa na shoo ya ukweli mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini Sam wa Ukweli, yaani ni usiku usio wa kawaida," alisema Mwilima.
Mwilima ambaye ni mtangazaji wa kituo cha runinga cha Star Tv, alisema maandalizi ya onyesho hilo yanaendelea vema na kuwataka mashabiki wa muziki kukaa mkao wa kula kupata uhondo toka kwa wakali hao.
Kundi hilo la Mapacha Watatu linaundwa na waimbaji hao toka bendi hasimu za African Stars 'Twanga Pepeta' na FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma'.
Mwisho
No comments:
Post a Comment