SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania, BFT, limeandaa kozi ya ukocha wa mchezo huo kwa vijana na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, ili kukuza na kuendeleza ngumi nchini.
Afisa Habari wa BFT, Eckland Mwaffisi, aliiambia Micharazo kuwa, kozi hiyo ya siku 10 inatarajiwa kuanza Desemba 14-24 ikifanyika jijini Dar es Salaam.
Mwaffisi alisema kozi hiyo itahusisha vijana wenye kupenda kufundisha mchezo huo, pia wangependa walimu wa shule za Msingi na Sekondari wajitokeze kwa wingi kwa sababu lengo lao ni kutaka kuusambaza mchezo huo shuleni kwa manufaa ya baadae kwa taifa.
"BFT katika mikakati yake ya kukuza na kuendeleza michezo kuanzia mitaani hadi shuleni imeandaa kozi ya siku 10 itakayowahusisha wote wenye 'idea' ya mchezo wa ngumi kwa lengo la kwenda kufundisha wenzao ili kuufanya mchezo huo urejee katika hadhi yake," alisema Mwaffisi.
Alisema tayari baadhi ya wanaopenda kushiriki kozi hiyo wameshaanza kujitokeza na alizidi kutoa wito kwa wenye kuhitaji kujifunza ukocha wa ngumi kujitokeza mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine, Kocha wa Ngumi wa Klabu ya Ashanti, Rajabu Mhamila 'Super D' amepewa msaada wa Sh. Laki 1.5 zitakazomwezesha kushiriki kozi ya siku 10 ya ukocha iliyoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT).
Msaada huo ambao ni wa pili kwa kocha huyo kupewa ulitolewa na mdau wa michezo Zulfiqal Ali kumwezesha Super D kufanikisha malengo yake ya kuendeleza mchezo wa ngumi kwa vijana
Akizungumza Dar es Salaam, wakati akimkabidhi pesa hizo Zulfiqal alisema ameamua kufanya hivyo ili kuungana na wadau wengine wa michezo ikiwemo serikali katika kuendeleza michezo.
Hata hivyo Zulfiqal amewaomba wadau wengine kujitokeza kuungana na jamii kusaidia kukuza michezo ili kuwawezesha vijana wasio na ajira waweze kujiajili.
Naye Super D alisema anashukuru na kuahidi kuzingatia kozi hiyo siku zote ili aweze kupanua ujuzi ambao utawawezesha kuwasaidia mabondia wanaochipukia hapa nchini.
Awali kocha huyo alipewa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi laki tatu na zaidi kwa ajili ya mazoezi ya mabondia wanaohudhuria mafunzo yanayotolewa na kocha huyo
No comments:
Post a Comment