STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

Coast Modern wapika albamu ya nne



BAADA ya kutamba na albamu yao ya 'Damu Nzito', kundi mahiri la muziki wa taarab la Coast Modern 'Watafiti wa Mipasho', limeanza maandalizi ya albamu yao mpya ya nne ikiwa imeshakamilisha nyimbo zipatazo tatu hadi sasa.
Mkurugenzi wa kundi hilo, Omar Tego 'Special One' aliiambia MICHARAZO kuwa, nyimbo tatu kati ya nne zinazolengwa kuwepo kwenye albamu hiyo ijayo zimeshakamilika kutungwa na kufanyiwa mazoezi tayari kupelekwa studio kurekodiwa.
Hata hivuo Tego alikataa kuzitaja nyimbo hizo kwa madai ni mapema mno na pia kuhofia asiibiwe 'idea' na wapinzani wake katika muziki huo wa taarab nchini.
"Tupo katika maandalizi ya kufyatua albamu yetu mpya itakayokuwa ya nne kwa Coast Modern, tayari tumekamilisha nyimbo tatu na tumesaliwa na mmoja, kuhitimisha nyimbo zitazotakiwa kabla ya kuzipeleka studio kurekodiwa," alisema Tego.
Tego alisema kwa jinsi walivyojipanga, huenda albamu hiyo ikakamilika na kuwa mitaani kabla ya Julai, kwani karibu kila kitu kimekamilisha wanachosubiri ni kuingia studio.
Alisema wataichelewesha kidogo albamu hiyo kutoka hadi Julai kwa nia ya kutoa nafasi ya albamu yao ya sasa ya 'Damu Nzito' kuendelea kutamba kwenye soko la muziki huo.
"Unajua tumeachia 'Damu Nzito' muda mfupi tu uliopita, hivyo ili kuipa nafasi ya kufanya vema sokoni, ndio maana tumepanga kuitoa albamu yetu ya nne kabla ya Julai," alisema Tego.
Kabla ya albamu hiyo ya 'Damu Nzito' kundi hilo la Coast Modern, liliachia albamu mbili zilizotikisa muziki wa mwambao nchini za 'I'm Crazy For You' na 'Kupendwa Isiwe Tabu' iliyokuwa na kibao kilichotamba cha 'Chongeni Fenicha Sio Maneno' ulioimbwa na Tego.
Aidha Tego, alisema kundi lao linaendelea kuzitambulisha nyimbo zao mpya na zile za albamu zao zilizopita katika maonyesho yao, ambapo kila Ijumaa huwa kwenye ukumbi wa Kiburugwa Inn, Mbagala na Jumamosi ufanya makamuzi yao Bashnet Hall, Mtoni Mtongani, jijini Dar es Salaam.

Mwisho

No comments:

Post a Comment