ONYESHO la 'Usiku wa Naksh Naksh wa Mwambao na Mastaa wa Muziki na Filamu', litakuwa ni pambano lisilo rasmi la kundi la Jahazi Modern Taarab na bendi ya Manchester Musica.
Kwa mujibu wa mraribu wa onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Travertine, Abdallah Mensah, makundi hayo mawili yataonyeshana umwamba mbele ya mashabiki watakoenda kulishuhudia.
Mensah, alisema tayari makundi hayo yameshaanza kutoleana tambo juu ya kufunikana siku ya onyesho hilo, ambalo litahusisha mastaa wengine kibao wa muziki akiwemo Prince Mwinjuma Muumin, aliyepo Africana Stars 'Twanga Pepeta'.
"Japo ni onyesho la kutoa burudani kwa kushirikisha wasanii mbalimbali nyota wa muziki na filamu, lakini ni kama mpambano wa Jahazi Modern Taarab na Manchester Musica, moja ya bendi zinazokuja juu kwa sasa nchini kwenye muziki wa dansi," alisema Mensah.
Wengine watakaopamba onyesho hilo litakalofanyika Mei 8 ni pamoja na Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Kopa, Mwanaidi Shaaban, Hassani Ally, Maua Tego, Thabit Abdul na kundi la Kanga Moja 'Ndembendembe.'
Pia wasanii wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella, Said Chegge pamoja na wakali wa filamu ambao bado wameweka kapuni kwa sasa nao watajumuika pamoja kuwapa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake burudani ya aina yake kwa wakati mmoja.
"Unaweza kuona mchanganyiko uliopo siku ya onyesho hilo, utakavyoweza kuwapa burudani zaidi ya moja kwa wakati mmoja, maana mbali ya taarab na dansi, pia wasanii mbalimbali wa filamu na muziki wa kizazi kipya watakuwepo kutoa burudani kabambe," alisema Mensah.
Mensah, alisema kwa sasa anahaha kusaka wadhamini wa onyesho hilo, ili kulizidishia manjonjo kabla ya kufanyika kwake.
Mwisho
No comments:
Post a Comment