STRIKA
USILIKOSE
Friday, April 15, 2011
Mwalubadu: Kujituma kumenipa tuzo 2010
ANAFAHAMIKA zaidi kama 'Mwalubadu', ingawa jina lake halisi ni Athuman Mussa Masangula, mmoja wa wachekeshaji mahiri nchini ambaye kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mgulani, jijini Dar es Salaam.
Mwalubadu alisema alianza kushiriki maigizo shuleni kwa kuigiza sauti za walimu wake na baadhi ya viongozi maarufu, huku akishiriki pia katika uchezaji ngoma na michezo mbalimbali.
Alikiendeleza kipaji chake hata alipokuwa Shule ya Sekondari Mzalendo, iliyopo Moshi, Kilimanjaro ambapo alikuwa akikodishwa kwa ajili ya kunogesha sherehe mbalimbali za harusi na kipaimara na kuzidi kupata umaarufu zaidi hadi alipomaliza masomo yake na kurejea Dar.
Alijiendeleza kielimu kwa kusomea masomo ya IT ngazi ya cheti pale Chuo Kikuu Mlimani, kitengo cha Kompyuta, huku akijishughulisha na masuala ya sanaa kupitia kundi la Katavi lililowahi kutamba na michezo ya kuigiza kiup[itia kituo cha ITV.
Baadhi ya michezo aliyoshiriki akiwa na kundi hilo yaliyomtambulisha kwa mashabiki ni 'Jabali', 'Miale' na 'Tunduni' kabla ya kuangukia kwenye filamu akiigiza 'Copy' mwaka 2007 na kufuatiwa na nyingine zikiwemo za vichekesho zilizomjengea jina kubwa nchini.
Mwalubadu ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo cha Radio cha Ebony FM iliyopo, Iringa, alisema alijikuta akipenda sanaa ya uigizaji na hasa vichekesho kwa kuvutiwa na Steve Urkel, aliyetamba na 'Family Matters' na Brian Deacon, aliyeigiza filamu kadhaa ya Yesu.
Alisema kujibidiisha na kujifunza kwa waliomtangulia kwenye fani ndiko kulikomfanya anyakue tuzo ya Mchekeshaji Bora wa mwaka 2010, kupitia mtandao wa Filamu Central.
Mkali huyo anayependa kucheza soka, muziki na kuangalia filamu za vichekesho, alisema pamoja na mafanikio aliyoyapata kwenye fani hiyo, bado hajaridhika na anajibidiisha zaidi ili zweze kuwa msanii wa kimataifa, akimiliki kampuni yake mwenyewe sambamba na kujiendeleza kielimu.
Baadhi ya kazi za filamu alizoshiriki na kumjengea jina kubwa katika fani hiyo nchini ni pamoja na 'Sheria', 'Lango la Jiji', 'Inye' na 'Kaka Ben' za vichekesho, huku filamu za kawaida ni 'The Strangers', 'Swahiba', 'Solomba' na nyinginezo.
Mbali na kuchekesha, Mwalubadu pia ni mtunzi na mwandishi wa filamu hizo, moja ya kazi yake binafsi ni 'King Mwalubadu'.
Mkali huyo aliyezaliwa Januari 10, miaka kadhaa iliyopita akiwa mtoto wa tatu wa familia ya Mzee Mussa Masangula, alisema hakuna jambo la furaha kwake kama siku alipoanza kutangaza katika kituo cha Ebony Fm, huku tukio la huzuni ni kufiwa na baba yake mzazi, kitu alichodai akisahau.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment