STRIKA
USILIKOSE
Friday, November 18, 2011
Banka afichua kilichompeleka JKT Ruvu
KIUNGO mahiri wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Mohammed Banka ametua JKT Ruvu akisema ni klabu aliyokuwa akiiota kwa muda mrefu kutokana na na kuwa na soka la kuvutia na lenye ushindani uwanjani.
Aidha amekanusha kuwahi kufanya mazungumzo na viongozi wa timu za Coastal Union na Moro United ili ajiunge navyo kama ilivyokuwa ikiripotiwa.
Akizungumza na MICHARAZO Banka, alisema tayari ameshamwaga wino wa kuichezea JKT kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na amefurahi mno.
Banka, alisema soka la JKT ndilo lililomsukuma kujiunga akiamini namna ya uchezaji wa klabu hiyo na aina ya wachezaji anaoungana nao itamsaidia kurejea upya katika soka la Tanzania baada ya nusu msimu kuwa nje ya dimba kutokana na mzozo wake na Simba.
"Nimemwaga wino wa kuichezea JKT Ruvu, kikubwa kilichonivutia kujiunga na timu hii ni aina ya soka inalocheza na wachezaji iliyonayo, ni kati ya klabu nilizokuwa naota kuzichezea kwa vile ni timu yenye malengo na ushindani wa kweli dimbani," alisema Banka.
Alipoulizwa imekuwaje amezitosa Coastal Union na Moro United ambazo zimekuwa
zikijinasibu kumnyemelea, Banka, alisema zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari
hakuwahi kufuatwa na kiongozi yeyote wa timu hizo kuzungumza nao.
"Ndugu yangu sijawahi kufuatwa wala kuwasiliana japo kwa simu kuzungumza kuhusu
kujiunga na klabu hizo, zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba natakiwa nazo, ila JKT Ruvu kabla ya kujiunga nilishafanya nao mazoezi weakati duru la kwanza likielekea ukingoni," alisema Banka.
Banka, aliyewahi kuichezea Moro United na aliyekuwa mchezaji wa Simba kabla ya kuigomea klabu hiyo kumtoa kwa mkopo kwa klabu ya Villa Squad ni miongoni mwa wachezaji watano wapya waliongezwa katika klabu hiyo ya JKT Ruvu.
Wengine waliotua JKT Ruvu ni George Mketo na Paul Ngahyoma toka Kagera, Said Hamis toka Polisi Morogoro na Bakar Kondo aliyerejeshwa kikosini.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment