STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 18, 2011

Niyonzima aikana Simba, awatroa hofu Jangwani



KIUNGO nyota wa kimataifa wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima 'Fabregas' amewatoa hofu wanayanga kwa kuweka wazi kwamba hana mpango wa kujiunga na mahasimu wao Simba kwa kile alichodai anaridhika na maisha yake Jangwani.
Pia, kiungo huyo alisema kama ni kuondoka Yanga, basi sio kwa kujiunga na klabu nyingine ya Tanzania, bali ni kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, ikiwa ni kati ya ndoto anazoota kila siku maishani mwake.
Akizungumza moja na kipindi cha michezo cha Radio One 'Spoti Leo', Niyonzima, amedai kushangazwa na taarifa kwamba Simba inamnyemelea wakati hajawahi kufanya mazungumzo yoyote na uongozi wa klabu hiyo au mtu yeyote.
Kiungo huyo aliyetua Jangwani akitokea klabu ya APR ya Rwanda, alisema mbali na kutowahi kuzungumza na mtu yeyote ili kujiunga Simba, lakini yeye binafsi hana mpango huo kwa vile anaridhika na maisha yake ndani ya klabu yake ya sasa.
"Aisee sina mpango wa kuihama Yanga na hivyo nawataka wanayanga wasiwe na hofu nadhani yanayosemwa yanatokana na kuvutiwa na soka langu, lakini sijawahi kuzungumza na mtu yeyote kujiunga Simba," alisema.
"Pia kwa namna mambo yangu yanayotekelezwa ndani ya Yanga na mie kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio, sioni sababu ya kutaka kuhama na kama ikitokea hivyo basi ni kwenda zaidi ya Tanzania, lakini sio kujiunga Simba," alinukuliwa Niyonzima.
Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya nchi yake ya Rwanda 'Amavubi' alisema ingawa yeye ni mchezaji na lolote linaweza kutokea, lakini hadi wakati akizungumza hakuwa amewaza lolote juu ya kuiacha Yanga aliyosaini nayo mkataba wa miaka miwili.
Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kwamba Simba imekuwa ikimwinda kiungo huyo ambaye soka lake limewakuna wengi tangu atue Jangwani, ikiwa kama jibu la watani zao, Yanga kudaiwa kumnyatia mshambuliaji wao, Felix Sunzu.
Tetesi hizo za Yanga na Simba kubadilishana wachezaji zimekuja wakati mbio za usajili wa dirisha dogo nchini likizidi kupambana moto.

Mwisho

No comments:

Post a Comment