BONDIA mahiri wa ngumi za kulipwa wa mkoa wa Morogoro, Mohamed Jeilani anatarajiwa kupanda ulingoni kuonyeshana ubabe na Mohammed Matimbwa wa Dar katika pambano lisilo la mkanda litakalofanyika siku ya Desemba 3, mjini Morogoro.
Pambano hilo la raundi nane litafanyika kwenye ukumbi wa Urafiki na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Mkurugenzi wa kampuni ya BS Promotion, waandaaji wa pambano hilo, Daudi Julian aliiambia MICHARAZO kwamba mchezo huo ni wa uzani wa kilo 60 na lengo lake ni kuhamamisha mchezo wa ngumi mkoani humo.
Julian, alisema maandalizi ya pambano hilo na michezo yote ya utangulizi yanaendelea vema na tayari mabondia wote watakaopigana siku hiyo wanaendelea kujifua kujiweka tayari kuonyeshana kazi ulingoni.
Aliwataja mabondia watakaowasindikiza Jailan na Matimbwa siku ya pambano lao ni pamoja na Maneno William ‘Chipolopolo’, Nassib Msafiri ‘Ngumi Nondo’ na Said Idd ‘Simple Boy’ watachapana na mabondia kutoka Dar es Salaam na Tanga.
"Kampuni yetu imeandaa pambano la ngumi la kirafiki kati ya Mohammed Jailan dhidi ya Mohammed Matimbwa litakalofanyika Desemba 3 mwaka huu na kusindikizwa na michezo mingine kati ya mabondia wa Moro dhidi ya wale wa Dar na Tanga," alisema.
Alisema mbali ya pambano hilo, kampuni hiyo pia inatarajia kuandaa mapambano mengine ya ngumi , siku ya kusherehekea sikukuu ya X-mass ambapo mabondia wa mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma na Tanga wataonyeshana kazi.
Julian ametoa wito kwa wafadhili wa michezo kujitokeza na kudhamini mapambano mbalimbali yatakayoandaliwa na kampuni yake kwa lengo la kuhamasisha mchezo huo mkoani humo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment